WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jaffo amezitaka Taasisi zilizo chini ya Wizara yake kufanya kazi kwa bidii, maarifa na kasi katika kiwango kinachothibitika wakati wakiepuka kuwa kikwazo katika kuwahudumia wafanyabiashara.
Dkt. Jafo ameyasema hayo Julai 15, 2024 wakati akiongea na Menejimenti ya Wizara, Wakuu wa Taasisi na Wenyeviti wa Bodi zilizo chini ya Wizara hiyo katika Kikao Kazi kilichofanyika, Julai 15, 2024 Dar es Salaam.
Aidha, Dkt Jafo amewataka Wakuu hao wa Taasisi kufanya kazi kwa ushirikiano ndani ya Taasisi, baina ya Taasiai na kati ya Taaaisi na Wizara huku wakiepuka kuwa miungu watu na kuwajali wafanyakazi wa ngazi za chini hadi juu ili kufanya kazi kwa ufanisi na tija na kutimiza Malengo ya Wizara hiyo ambayo ni muhimu katika ujenzi wa uchumi.
Katika hatua nyingine, amewataka Wenyeviti wa Bodi za Taasisi hizo kufuatilia hoja zote za CAG zinazohusiana na Taasisi zao kuzifanyia kazi na kutoa taarifa kwake ndani ya mwezi mmoja.
Aidha, amelitaka Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ndani ya mwezi mmoja kufuatilia na kutoa taarifa yenye sababu pamoja na mapendekezo ya nini kifanyike ili kuuwezesha Mradi wa Liganga na Mchuchuma pamoja na ule wa Magadi Soda unaotarajiwa kuongeza ajira na Pato la Taifa kuanza mapema iwezekanavyo.
Dkt Jafo pia ameielekeza Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi Ghalani (WRRB) kufuatilia maghala yote nchini na kujua bidhaa zinazoingia na jinsi zinavyochangia ukuaji wa uchumi kwa kuwa Maghala yana fusa kubwa katika kukuza uchumi.
Vile vile amelitaka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Kufuatilia, kutoa ushauri na mkakati wa kutumia maeneo na viwanja vyote vilivyotengwa kwa ajili ya matumizi ya Shirika hilo.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na Menejimenti ya Wizara, Wakuu wa Taasisi na Wenyeviti wa Bodi za Taasisi ziilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara. Kikao kazi hicho kimefanyika Julai 15, 2024 katika Ofisi za TANTRADE Jijini Dar es Salaam.
Menejimenti ya Wizara, Wakuu wa Taasisi na Wenyeviti wa Bodi za Taasisi ziilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara wakiwa kwenye kikao kazi cha Waziri wa Viwanda na Biashara kilichofanyika Julai 15, 2024 katika Ofisi za TANTRADE Jijini Dar es Salaam.
(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)