Njombe. Wafanyabiashara wa mazao katika Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe wamepewa siku saba kuanzia leo kuondoka maeneo yasiyo rasmi na kuhamia Soko la Kiumba lililojengwa maalumu kwa ajili yao.
Agizo hilo limetolewa leo Jumanne Julai 16, 2024 na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Makambako, Keneth Haule wakati akizungumza na wafanyabiashara hao.
Wafanyabiashara hao wamepewa agizo hilo ikiwa ni siku saba zimepita tangu Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka awatake wafanyabiashara 112 walioingia ubia na halmashauri hiyo kujenga soko la mazao Kiumba kuhamia sokoni humo bila kuwaathiri wenye mitaji midogo.
Haule amesema wamekubaliana soko la mazao ya nafaka liwe Kiumba na wameshirikiana kukamilisha na lipo tayari kwa biashara kufanyika.
Amesema soko hilo lililogharimu Sh1.1 billioni, wafanyabiashara wametoa zaidi ya Sh900 milioni kwa ajili ya ujenzi na likatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.
Haule amesema Mji wa Makambako hautakiwi kuwa na maghala yasiyo rasmi, hivyo mazao yote ya nafaka yatapatikana kwenye Soko la Kiumba.
Amesema magari yote yanayobeba viazi yanatakiwa kushusha bidhaa hiyo katika Soko la Magegele huku matunda yakitakiwa kushushwa Soko la Maguvani.
“Utekelezaji huo uanze mara moja wapo watauliza magari makubwa, lakini yote hayatakiwi kuingia katika soko hilo bila kujali limebeba viazi, vitunguu au nafaka,” amesema Haule.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Makambako, Hanana Mfikwa amesema baada ya wiki moja kupita kazi ya kuzuia magari kutoshusha mazao soko kuu itaanza na kwa wale watakaokiuka watatozwa faini ya Sh200,000 hadi Sh1 milioni.
“Tuanze kuhama kwa hiari kuanzia leo kwa wiki moja baada ya hapo tutazuia kushusha mizigo kwenye masoko mengine na atakayevunja sheria tutampiga faini,” amesema Mfikwa.
Ofisa Biashara wa Halmashauri ya Mji wa Makambako, Caros Mhenga amesema hali hiyo itasaidia kuupanga mji na kutanua wigo wa biashara kwa wananchi.
“Huku mjini utaruhusiwa kubeba mazao endapo umebeba kwenye bodaboda au guta kwa ajili ya kupeleka soko kuu au Maguvani zaidi ya hapo ni marufuku,” amesema Mhenga.
Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha Mji wa Makambako unajengeka na kupangika vizuri na kufanya hivyo hakuna zaidi ya wananchi wenyewe na wafanyabiashara.
Mmoja wa wafanyabiashara hao, Michael Sanga amesema wamekubaliana na agizo hilo huku wakiitaka halmashauri kuboresha miundombinu hasa ya barabara ndani ya soko pamoja na huduma ya mawasiliano kwa kujenga mnara ili kurahisisha biashara zao.