Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linawatangazia wateja wake kuwa kutakua na katizo la umeme. Sababu ya katizo ni kuzimwa kwa njia kuu ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 220 kutoka Msamvu, Morogoro hadi Dodoma (SGR) ili mkandarasi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kufanya kazi zilizokuwa zimebaki kwenye vituo vya treni vya msongo wa kilovoti 220/33.
Baadhi ya wateja wa Mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma, Mbeya, Songwe, Singida, Shinyanga, Simiyu, Tabora, Mwanza, Mara, Geita, Arusha, Kilimanjaro na Manyara , siku ya Jumatano Tarehe 17 Julai 2024 na Alhamisi, Tarehe 18 Julai 2024 Kuanzia saa 02:00 Asubuhi – 12:00 Jioni
Lengo la kazi hiyo ni kuunganisha mifumo ya mawasiliano kwa ajili ya uongozaji na ufuatiliaji wa treni kwa kuunganisha miundombinu ya mawasiliano kati ya vituo vya kupoza umeme wa treni na vituo vikuu vya uendeshaji vilivyopo Dar es Salaam (Operational Control Centre 1- OCC1) na Morogoro (Operational Control Centre 2- OCC2)
Kufanyika kwa zoezi hilo pia kutaiwezesha TRC kuimarisha uendeshaji na ufuatiliaji wa treni na kuimarisha ufuatiliaji (monitoring) na uendeshaji (operations) wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 220 kutoka Msamvu Morogoro hadi Dodoma (SGR).