KAMA hatasimama kidete, basi madogo janja Jannik Sinner na Carlos Alcaraz watamchelewesha sana kama sio kufuta nafasi yake ya kuweka rekodi mpya ya dunia ya mataji 25 makubwa ya tenisi (Grand Slam) anayoisaka supastaa wa tenisi, Novak Djokovic.
Djokovic mambo sio mambo mwaka huu kwani ameshindwa kubeba taji lolote kubwa katika yale matatu makubwa ya dunia (Grand Slam) kuanzia lile la Australia aliloachia mikononi mwa Jannik Sinner na mawili ya Ufaransa (Rolland Garros) na Wimbledon yaliyochukuliwa na Alcaraz.
Mserbia Novak, baada ya kupoteza fainali ya pili mfululizo ya Wimbledon mbele ya Alcaraz Jumapili iliyopita, alikiri kuwa ni ngumu kwake kupambana na vijana wapya kina Alcaraz na Sinner ambao bado wana njaa na nguvu ya kucheza mchezo huo wakiwa na miaka 21 kwa 22 mtawalia.
Hii inamfanya staa huyo kuwa njiapanda kutimiza lengo la kufikisha mataji 25 ya tenisi duniani yale makubwa ambapo kwa sasa anasimama na rekodi ya mataji 24 kama Margaret Court wakati yeye anahitaji kufikisha mataji 25, na ana kazi ya kufanya kwenye Olimpiki nchini Ufaransa pamoja na taji la Marekani (US Open).