KAYA LAKI NNE AMBAZO SASA MAMBO YAO SAFI KUONDOLEWA KATIKA TASAF

Na Said Mwishehe,Michuzi TV- Arusha

MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umesema unatarajia kuziondosha kaya masikini 400,000 ambazo zimeimarika kiuchumi kiasi cha kuwa na uhakika wa kumudu milo mitatu kwa siku.

Kwa mujibu wa TASAF kaya hizo zitaondolewa Septamba mwaka huu na hiyo ni baada ya kufanyika kwa tathimini kuhusu wanufaika wa Mfuko huo ambapo kwa sasa wanaoweza kujimudu kiuchumi.Kaya hizo wakati zinaingizwa katika Mfuko huo walikuwa na hali duni kiuchumi na wengine kutomudu milo mitatu kwa siku achilia mbali mahitaji ya msingi.

Akizungumza mbele ya waandishi na Wahariri kabla ya kutembelea wanufaika na miradi ya maendeleo katika elimu,afya,miundombinu na maji , Mkurugenzi Mtendaji wa wa TASAF Shedrack amesema pamoja na mafanikio makubwa ya Mfuko huo katika kuwezesha Kaya masikini kwa sasa wako katika tathimini ili kuondoa kaya ambazo hali zao kiuchumi zimeimarika.

Amefafanua kutokana na tathimini waliofanya inaonesha kati ya kaya milioni 1,370,000 ambazo zipo katika mpango wa kuwawezesha kiuchumi kutokana na kukabiliwa na umasikini uliokithiri lakini ni kupitia mfuko huo kaya 400,000 zitaondolewa.

“Tunatarajia kuziondoa kaya 400,000 na hii ni baada ya kufanyika tathimini na kubaini sasa wanaweza kujiendesha kiuchumi , baada ya kuwa katika Mfuko wa TASAF na kunufaika na miradi mbalimbali na fedha walizokuwa wakipatiwa hivi sasa wameimarika kiuchumi, mambo yao safi kwani wanajimudu kiuchumi.

“Tunafahamu katika kuondoa kaya hizo wakati utakapofika mtasikia malalamiko maana mtu ameshazoea kupewa fedha za TASAF akiambia anaondolewa hawezi kukubali,ingawa wengine wako tayari kwani wanaona kabisa maisha Yao yamekuwa bora ukilinganisha na awali kabla ya kuingizwa TASAF.”

Mziray amesema baada ya kuziondoa kaya hizo watakuwa wamebakiwa na kaya 900,000 ambazo zitaendelea kuhudumiwa na Mfuko huo huku akieleza pamoja na kuondoa kaya 400,000 Kuna kaya nyingine kwa hali ya umasikini walionao hawawezi kutoka leo Wala kesho ingawa kimsingi wanufaika wanatakiwa kufahamu hakuna anayeweza kuhudumiwa na mfuko huo milele.

Hata hivyo amesema kukamilika kwa Awamu ya tatu ya TASAF kumekuwa na mafanikio makubwa kutokana na jitihada za Serikali kusaidia kaya masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii huku akifafanua mafanikio ya mfuko yametokana na ushirikiano uliopo katika halmashauri mbalimbali ambazo wamekuwa wakitekeleza miradi.

Kuhusu miradi ya maendeleo inayoibuliwa na Wananchi, amesema Mfuko kupitia programu ya kusaidia katika miradi ya maendeleo, amesema kwa Mkoa wa Arusha Kuna miradi inayoendelea kutekelezwa ikiwemo miradi katika ekta ya afya, elimu na maji

Amesema miradi hiyo inatekelezwa kwa kushirikiana na watalaamu wa halmashauri ambazo zinatekeleza miradi ya TASAF na kwa sasa halmashauri 186 nchini zinatekeleza miradi ya kimaendeleo.




Related Posts