Filamu 70 zapenya Tamasha la ZIFF

Dar es Salaam. Filamu 70 zitachuana kuwania tuzo kwenye tamasha la 27 la Kimataifa la Filamu la Zanzibar (ZIFF) litakaloanza Agosti mosi hadi 4 visiwani Zanzibar.

Filamu hizo ni kati ya 3,000 zilizopokewa kutoka mataifa mbalimbali duniani na 70 kupenya kwenye mchujo.

Filamu za Afrika Mashariki zilizowasilishwa zilikuwa 354 ambazo kutoka Kenya ni 169, Uganda filamu 123, Tanzania 62 Rwanda 12 na Burundi filamu tatu. Afrika Kusini iliwasilisha filamu 71.

Mkurugenzi wa tamasha hilo, Hatibu Madudu amesema filamu nyingine zilizowasilishwa zilitoka kwenye mataifa zaidi ya 100.

“Filamu zote 3,000 zilitazamwa na majaji 70 kutoka mataifa mbalimbali katika mchujo uliobakisha 70 zilizoingia kwenye kinyang’anyiro,” amesema.

Amesema, vipengere 11 tofauti vitawaniwa kikiwamo cha tamthilia bora. Katika kipengere hicho kilichoingiza tamthilia 10, tano ni za Kitanzania.

Tamthilia za Tanzania zilizoingia kwenye kinyang’anyiro ni Bunji, Twisted, Ripoti, Juakali na Dhohari.

Kwenye kipengele cha filamu makala (documentary) kati ya 13 zilizochaguliwa tatu ni za Kitanzania.

Akizungumzia maandalizi ya tamasha hilo linalofanyika kwa mara ya 27 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1997, ofisa mtendaji mkuu wa ZIFF, Joseph Mwale amesema litakuwa pia na majukwaa mbalimbali.

Ameyataja kuwa ni jukwaa la watoto na wanawake, pia litakuwa na mbio za ngalawa, mpira wa miguu wa wanawake wa ufukweni, majadiliano na majukwaa ya wazi ya uonyeshaji wa filamu.

Amesema ili kushiriki katika majukwaa hayo, inapaswa kujisajili kuanzia Julai 20 hadi 25.

Hata hivyo, Mwale amefafanua kwamba tofauti na misimu iliyopita msimu huu hakutakuwa na mashindano ya filamu za Sembene Ousmane ambayo awali yaliungwa mkono na Deutsche Gesellschaft für Internationale Entwicklung (GIZ).

“Hayatofanyika mwaka huu kutokana na kujiondoa ghafla kwa mfadhili katika hatua za mwisho, wasimamizi wa tamasha wamepeleka ombi kwa GIZ kuwaomba wafikirie tena uamuzi wao angalau kwa mwaka huu, huku tukiendelea kutafuta msaada kutoka kwa wafadhili wengine wenye uwezo wa kuchukua udhamini huo,” amesema.

Vipengele vingine vinavyoshindaniwa ni cha filamu bora ya Urefu, Filamu Bora ya Hali Halisi, Tuzo ya Emerson kwa Filamu Bora ya Zanzibar, Filamu bora Fupi au Katuni Bora, Filamu Bora ya Afrika Mashariki, Mwigizaji Bora (Afrika Mashariki).

Pia, kuna Mwigizaji Bora wa Kike (Afrika Mashariki), Mwigizaji Bora (Tanzania), Mwigizaji Bora wa Kike (Tanzania), Tuzo ya Mwenyekiti wa ZIFF na Tuzo ya Mafanikio ya Maisha pamoja na Tuzo ya Chaguo la Watu.

Mwale amesema mchakato wa upigaji kura kwenye kipengele hicho utaanza Julai 20 hadi Agosti 3.

Amebainisha ZIFF itakuwa na programu ya siku ya kitaifa ya Zanzibar Julai 31 2024, “Ikiwa ni sehemu ya tukio la kabla ya tamasha tunatarajia kuonyesha filamu za Zanzibar,”amesema Mwale.

Related Posts