Nairobi. Polisi katika Mji Mkuu wa Kenya, Nairobi leo Julai 16, 2024 wametumia gesi ya machozi kuwatawanya waandamanaji wa Gen Z wanaopinga Serikali na kumtaka Rais William Ruto ajiuzulu.
Kwa mujibu wa Aljazeera, majeruhi wameripotiwa Nairobi na sehemu nyingine, huku mwandamanaji mmoja ameripotiwa kuuawa huko Kitengela.
Shirika la Habari la Reuters limeripoti kwamba polisi huko Kitengela walifyatua risasi kwa waandamanaji waliokuwa wakirusha mawe, wakichoma matairi na kuimba “Ruto lazima aondoke.”
Mwandishi wa Reuters ameeleza kuuona mwili wa mwandamanaji ukiwa umelala chini na damu ikivuja kutoka kwenye jeraha la kichwa.
Awali, maandamano hayo yaliyoanza mwezi mzima uliopita yalilenga kupinga Muswada wa Fedha 2024 uliodaiwa kuongeza kodi uliopitishwa na Bunge la Kenya.
Baada ya maandamano hayo kukolea, Rais wa Kenya, William Ruto aliondoa muswada huo na kufanya mabadiliko ikiwa pamoja na kuvunja baraza lake la mawaziri.
Hata hivyo, maandamano hayo sasa yamechukua sura nyingine, sasa waandamanaji wanataka Rais Ruto aondoke madarakani.
Maandamano hayo yanayoratibiwa na vijana maarufu kwa jina la Gen Z wakitumia teknolojia za mawasiliano kuyaratibu.
Hata hivyo, maandamano hayo yamekuwa yakijibiwa na polisi walijibu kwa mabomu ya machozi, mizinga ya maji na risasi za moto na kusababisha vifo vya waandamanaji 39.
Ford Foundation yakana kufadhili maandamano
Shirika la Ford Foundation la Marekani limekanusha madai ya Rais Ruto kwamba lilifadhili maandamano ya kupinga serikali nchini Kenya.
Katika taarifa rasmi iliyonukuliwa na mtandao wa Nation, shirika hilo lisilo la kiserikali (NGO) limesema halifadhili shughuli kama hizo.
“Hatujafadhili au kudhamini maandamano ya hivi karibuni dhidi ya muswada wa fedha na tuna sera kali ya kutokuwa na upendeleo kwa misaada yetu yote,” amesema Tolu Onafowokan, mkurugenzi wa mawasiliano ya kimkakati wa shirika hilo akiijibu nation.africa.
Rais Ruto, akiwa katika ziara ya maendeleo Nakuru Jumatatu ameitaka NGO hiyo kufichua wafadhili wowote wa kigeni na waandaaji wa maandamano ya kupinga Serikali, akitaja kwa jina Ford Foundation. Ameonya kuwa wale waliohusika na maandamano hayo watakabiliwa na hatua za kisheria.
“Tunaiomba Ford Foundation kueleza Wakenya nafasi yake katika maandamano ya hivi karibuni. Kama hawana nia ya demokrasia Kenya, wanapaswa kujirekebisha au kuondoka. Tutawaita wale wote wanaokusudia kurudisha nyuma demokrasia yetu iliyopatikana kwa bidii,” alisema Rais Ruto.
“Wakati tunakubali haki ya Wakenya kuandamana kwa amani kwa ajili ya kutetea nchi ya haki na usawa, tunakana matendo yoyote au matamshi yanayochochea chuki au vurugu dhidi ya taasisi yoyote, mtu binafsi, au jamii.
“Kama tulivyobainisha wakati wa ziara ya Serikali ya Kenya nchini Marekani Mei, tumejitolea kujenga kwenye urithi wa zaidi ya miaka 60 wa Ford Foundation katika eneo hili ili Wakenya waweze kufungua fursa zinazowafikia wote,” ilisoma taarifa hiyo.
“NGO hiyo pia ilisisitiza ahadi yake ya kihistoria na inayoendelea kwa Kenya tangu 1963, ikiwamo msaada kwa watumishi wa umma, wataalamu wa kiufundi, sekta ya elimu na mipango mbalimbali ya mashirika ya kiraia.
“Tunaendelea kujitolea kusaidia kazi katika kusaidia maendeleo ya Kenya na uongozi wa Kenya katika hatua ya Afrika na kimataifa, iliyoonyeshwa na msaada wetu kwa mkutano wa kwanza wa hali ya hewa wa Afrika uliofanyika 2023 Nairobi na uongozi wa sasa wa Kenya kama mwenyekiti mwenza wa Ushirikiano wa Serikali Wazi,” amesema Onafowokan.
Imeandaliwa na Mashirika ya Habari.