Ma-DC Tanga wakabidhiwa magari mapya ya Sh683 milioni

Tanga. Wakati Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Buriani akiwakabidhi wakuu wa Wilaya za Pangani, Kilindi na Korogwe, viongozi hao wamesema yatarahisisha kazi ya kuwahudumia wananchi.

Magari hayo yaliyogharimu Sh683 milioni ni sehemu ya vyombo vya usafiri vilivyotolewa kwa Mkoa wa Tanga vikigharimu zaidi ya Sh1.1 bilioni.

Akizungumza katika hafla ya kuwakabidhi magari viongozi hao leo Jumanne Julai 16, 2024, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Buriani amempongeza mkuu wa wilaya ya Kilindi kwa kukusanya mapato kwa asilimia 130.

“Tutaomba waheshimiwa wakuu wa wilaya kila wiki mpite kwenye mifumo, mdai wakurugenzi wawapatie taarifa za kwenye mifumo muweze kujua fedha zinazokusanywa, zilizopo mikononi ninyi wastukizieni tu ikibidi kuanzia sasa ili kujua fedha zinazokusanywa kwenye maeneo yenu,” amesema Balozi Batilda.

Akizungumza baada ya kupokea gari lake, Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Hashim Mgandilwa amesema gari hilo limekuja kwa wakati kwa kuwa, gari alilokuwa akilitumia lilikuwa limechakaa.

“Ukitazama gari langu mheshimiwa mkuu wa mkoa, limetembea kilomita 437,822, nimepata gari hili jipya sasa ari itaongezeka ya utatuzi wa kero,na usimamizi wa miradi, lakini kupitia chombo hiki kipya hata migongo haitaleta shida,” amesema.

Amesema kuwa Wilaya ya Kilindi ina ukubwa sawa na robo ya Mkoa wa Tanga, hivyo amekuwa akipata changamoto za hapa na pale akiwa kwenye shughuli zake za kiutendaji ikiwamo kutatua changamoto za wananchi wa wilaya yake.

Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Mussa Kilakala amesema kupatikana kwa magari hayo kutawawezesha kuwafikia wananchi kwa wakati katika makundi mbalimbali, wakiwamo wazee, vijana na wajane.

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, William Mwakilema amesema watayatumia kwa uadilifu magari hayo, lakini pia kwasababu wameaminiwa basi, watahakikisha wanayatumia kama walivyoelekezwa.

Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga Seleman Sankwa kwa upande wake amewataka wakuu hao wa wilaya wasiyatumie magari hayo kwenye sehemu ambazo hayapaswi kuwepo na badala yake yatumike kama Serikali ilivyokusudia.

Related Posts