Mikopo ilivyo mwiba nchi za Afrika Mashariki

Dar es Salaam. Miongoni mwa masuala yanayowaumiza vichwa viongozi na wananchi wa nchi za Afrika Mashariki, ni ukubwa na mwenendo wa deni ambalo limegeuka mwiba katika mataifa hayo na hivyo umakini kuhitajika katika matumizi ya fedha zinazokopwa.

Kwa sehemu kubwa bajeti za kulipa madeni katika nchi hizo ama zimezidi au kukaribia nusu ya mapato yanayokusanywa na nchi hizo, hali inayoziweka njiapanda katika utekelezaji wa miradi yake ya maendeleo.

Hali hiyo, mbali na kuwashtua wananchi, pia imekuwa inawaweka njiapanda viongozi, huku wachumi wakionya juu ya matumizi sahihi ya fedha hizo na uwezekano wa kuwepo ongezeko la kodi.

Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan alimweleza Kamishina Mkuu mpya wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwa jukumu alilonalo ni kuhakikisha kunakuwa na ukusanyaji mzuri wa mapato ili nchi ipunguze kukopa.

“Tunachohitaji ni kupungua kukopa. Tunakopa, tunajichetua kwa kila anayekuja … World Bank (Benki ya Dunia) wanatunyanyasa tumo tu, kwa sababu tuna miradi ya maendeleo na pesa hatuna, hivyo tunalazimika kukopa,” alisema, mara baada ya kumwapisha Yusuf Mwenda kuongoza TRA.

Alisisitiza kuwa ndiyo maana Serikali imeweka mazingira mazuri ya kuvutia biashara na uwekezaji kumsaidia kamishna huyo kukusanya mapato ya ndani kwa sababu kukopa kuna kunyanyasika.

Kwa mujibu wa Japhet Justin, kamishina wa usimamizi wa Deni la Serikali wa Wizara ya Fedha, hadi Machi mwaka huu deni la Serikali nchini Tanzania lilikuwa Sh91 trilioni na la sekta binafsi Sh23.7 trilioni, hivyo jumla deni la Taifa lilikuwa Sh115 trilioni

“Ukubwa wa deni unakua kwa kuongozwa na shabaha za uchumi, Kunakuwa na malengo yanayopelekwa bungeni, mfano mwaka ujao tunasema tunataka kukopa kiasi fulani, hivyo bajeti iliyosomwa hivi karibuni inaenda kutengeneza matumizi na mapato tarajiwa kwa mwaka husika wa fedha,” alifafanua.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa deni hilo bado ni himilivu na kuwa ukopaji unasimamiwa na sheria ya mikopo na madeni na taratibu za kukopa zinafanyika kutokana na msingi ya sheria.

Bajeti ya Serikali mwaka huu wa fedha inaonyesha kuwa asilimia 30 ya bajeti itategemea mikopo na misaada, huku matumizi ya kulipa madeni kwa mwaka husika yakiwa Sh13.12 trilioni, ambayo ni sawa na asilimia 26 ya bajeti yote na asilimia 44.6 ya mapato ya kodi.

Sehemu kubwa ya Sh49.3 trilioni zilizopangwa kukusanywa na kutumika nchini zitatokana na mapato ya ndani ya Serikali Kuu ambayo ni Sh33.25 trilioni na karibu theluthi moja itakayobakia itategemea mikopo na misaada ambayo kwa ujumla itakuwa (Sh14.7 trilioni).

Nchini Kenya, Rais William Ruto alisema hivi karibuni katika mahojiano na wahariri kuwa amekuwa akifanya juhudi kubwa kuinusuru Kenya na mzigo wa madeni ambao umekua kwa kasi zaidi ndani ya miaka 10 iliyopita.

Alisema ili aweze kuendesha Serikali vizuri, mwaka huu wa fedha atalazimika kukopa Shilingi za Kenya trilioni 1 (Sh20.8 trilioni), lakini kwa kuongeza kodi nchi ingeweza kuepuka ongezeko hilo la mkopo ambao kwa sasa uwiano wake ni asilimia 68 dhidi ya pato la Taifa (GDP).

Ruto alisema kwa mwaka wa fedha uliopita, Serikali yake ilikusanya KSh2.3 trilioni (Sh47.9 za Tanzania) kutoka katika vyanzo vya kodi na kati ya kiasi hicho, KSh1.1 trilioni (Sh22.9 trilioni) kilitumika kulipa madeni, KSh1 trilioni (Sh20.8 trilioni) zikatumika kulipa mishahara.

“Kutokana na hilo, nchi ililazimika kwenda kukopa nje ili kuzilipa kaunti na kulipia huduma za kijamii. Sasa nakisi yetu baada ya muswada wa bajeti kutopita, itabidi badala ya kukopa KSh600 bilioni tuongeze zaidi karibu KSh1 trilioni (Sh22.9 trilioni za Tanzania),”

Katika mahojiano hayo, Ruto alisema kwa sasa nchi yake ipo katika hali mbaya ya kifedha na mwenendo huo bila kuongeza makusanyo ya fedha za ndani, nchini hiyo haitafikia hatua ya wananchi wake kujivunia wala kukua.

Alisema mwaka 2013 deni la Taifa la Kenya lilikuwa KSh1.8 trilioni (Sh36.97 trilioni za Tanzania), ndani ya miaka mitano likaongezeka hadi Sh11 trilioni (Sh225.96 trilioni) ambazo zimetekeleza miradi mingi ya maendeleo, lakini kwa mkopo.

“Leo hatuna utulivu wa kukopa tena, tumefikia ukomo na pesa yote tuliyokopa kuanzia kipindi hicho mikopo yake imeiva na hivyo imekuwa shida, kwani tunatumia Sh1.1 trilioni (Sh22.60 trilioni) kila mwaka kutoka katika fedha za walipakodi wa kawaida kwa ajili ya kulipa riba tu, kwani ukijumlisha na mkopo wenyewe inafika takribani Sh1.8 trilioni (Sh36.97 trilioni),” alisema.

Kwa upande wa Uganda, mwaka huu wa fedha imepanga kukusanya na kutumia USh72.13 trilioni (Sh51. trilioni za Tanzania), kati ya fedha hizo, USh32.2 trilioni (Sh23.13 trilioni za Tanzania) zitatokana na kodi za ndani, huku ikikopa Ush39.93 trilioni (Sh28.69 trilioni) katika vyanzo vinginevyo, ikiwemo mikopo na misaada.

Hata hivyo, Taifa hilo la nne kiuchumi ndani ya Afrika Mashariki, linatarajia kutumia Ush21.7 trilioni (Sh15.59 trilioni) kugharimia deni la Serikali ambalo limefika Ush96.1 (Sh69.04 trilioni) hadi mwaka 2023.

Bajeti ya Uganda kwa mwaka huu imeongezeka kwa kiwango kikubwa kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni kuiva kwa mikopo mingi, lakini pia utekelezaji wa miradi mingi ya maendeleo.

Kati ya fedha za kuhudumia deni la Serikali USh3.1 trilioni (Sh2.23 trilioni) ni kwa ajili ya kulipa deni, USh9.5 trilioni (Sh6.83 trilioni) malipo ya riba, USh19.8 trilioni (Sh14.23 trilioni) kwa ajili ya deni la ndani, USh 9.1 trilioni (Sh6.54 trilioni) zitalipwa kwa Benki ya Uganda na USh200 bilioni (Sh143.69 bilioni) zitalipa madai ya ndani.

Ukiacha nchi za Tanzania, Kenya na Uganda zinazoongoza kwa madeni, nchi inayofuata kwenye ukanda huo, ni Rwanda, ambayo deni lake ni Dola za Marekani 8 bilioni (Sh21.2 trilioni).

Inafuatia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambayo deni lake linatajwa kuwa Dola za Marekani 6.78 bilioni (Sh18 trilioni), ambalo uwiano wake kwa pato la Taifa ni asilimia 14.6.

Sudan Kusini yenyewe deni lake ni Dola 3.7 bilioni (Sh9.8 trilioni) ambalo ni asilimia 37.8 ya pato la Taifa, Burundi ina deni la Dola 954.2 milioni (Sh2.53 trilioni) huku deni la Somalia likiwa Dola 0.6 bilioni (Sh1.5 trilioni).

Akichambua hali ya madeni katika nchi za Afrika Mashariki, Profesa wa uchumi, Abel Kinyondo amesema changamoto ya mikopo kwa mataifa hayo inatokana na nidhamu yao ya matumizi.

“Matumizi ya Serikali nyingi hayaendani na uhalisia wake wa kiuchumi, ukiangalia hata ripoti za ukaguzi wa hesabu za Serikali unakuta kiasi cha fedha zinazopotea kupitia ubadhirifu ni kikubwa kuliko hata mikopo yenyewe,” amesema.

Profesa Kinyondo amesema mapato ya ndani yanayokusanywa yanatosheleza mahitaji ya mataifa mengi, hata kama si kwa asilimia 100, basi kwa kiwango kikubwa isipokuwa yanawekwa kwenye kapu lenye matobo.

“Tukidhibiti wizi hatutakuwa na sababu za kukopa, kama udhibiti wa matumizi sio mzuri hata wigo wa kodi ukiongezeka na mapato ya ndani yakaongezeka ni kazi bure, maana mikopo itaendelea na yenyewe ina uraibu wake ukianza hauachi,” amesema Profesa Kinyondo.

Kwa mujibu wa profesa huyo, madeni makubwa yanaathiri uwezo wa nchi kutekeleza miradi ya maendeleo na thamani ya sarafu, kwa kuwa mengi yapo kwa fedha za kigeni, hivyo fedha za ndani zinahaha kununua hizo za nje.

Profesa Kinyondo amesema ni muhimu nchi kuchukua tahadhari, kwani madeni yanapokuwa makubwa kuna hatari ya kuwekwa chini ya uangalizi ya Benki ya Dunia, kama ilivyokuwa kwa mataifa mengi miaka ya 1990.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Madeni na Maendeleo Tanzania, Hebroni Mwakagenda amesema kwa nchi zinazoendelea, zikiwemo za Afrika Mashariki, mikopo haiepukiki, ila ni muhimu kuwa na matumizi sahihi na kuongeza makusanyo ya ndani.

“Kila mwaka tunakuwa na ongezeko la bajeti, lakini utekelezaji wake hautimizwi sehemu nyingi, hata asilimia 60 ya kilichotengwa haifiki, hiyo ni kwa sababu tunatumia fedha nyingi kulipa deni badala ya shughuli zetu za maendeleo,” amesema.

Amesema hatari yake ni nchi kushindwa kutoa huduma za kijamii au kutoa kwa kiwango kidogo.

“Hapa sasa mambo kadhaa yanapaswa kuzingatiwa ili kuepuka madeni makubwa, kwani ni kuongeza wigo wa walipa kodi, kuongeza elimu ya kodi, kwani sasa mikopo tunayoichukua ina hatari zaidi kwa kuwa inatoka katika taasisi za kibiashara,” amesema Mwakagenda.

Related Posts