Watanzania  wenye matatizo ya afya waitwa kutibiwa ndani ya meli ya hospitali

Dar es Salaam. Watanzania wenye matatizo ya magonjwa ya ndani, kina mama, watoto na kuungua wametangaziwa fursa ya kwenda kutibiwa bure baada ya madaktari bingwa kutoka Jeshi la Ukombozi la Watu wa China kuwasili nchini.

Madaktari hao wamewasili na Meli ya Hospitali ya ‘Ark Peace’ yenye vifaa vyote vya kufanya uchunguzi wa kiafya na watafanya matibabu kwa Watanzania kwa siku tano, kuanzia Julai18 hadi Julai 23 mwaka huu.

Kwa siku watakuwa na uwezo wa kuhudumia watu 600 asubuhi 300 na jioni 300, hivyo kwa kipindi hicho wagonjwa 3,000 watanufaika na fursa hiyo.

Meli hiyo yenye namba 866 si mara ya kwanza kuja nchini, mwaka 2017 ilikuja na kutia nanga katika Bandari ya Dar es Salaam kisha kutoa huduma hizo kwa Watanzania.

Akikazia fursa hizo katika mapokezi ya meli hiyo yaliyofanyika leo Junanne Julai 16, 2024 katika Bandari ya Dar es Salaam, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema meli hiyo ni hospitali yenye kila kitu ndani yake vikiwamo vyumba vinane vya upasuaji.

“Ina helikopta inayotumika kukimbiza wagonjwa mahututi na ina ICU zaidi ya moja na kuna wodi mbalimbali za magonjwa ya ndani, kina mama, watoto na madaktari mabingwa kutoka China kwa kushirikiana na Jeshi la Tanzania watakuwa wanatoa matibabu ndani ya meli hii,”amesema.

Chalamila amesema pia kutakuwa na jopo lingine litakalokuwa na jukumu la kuzunguka kuanzia Julai 18 katika hospitali mbalimbali huku akieleza kwa kutambua hilo wameweka utaratibu kwa viongozi wa Serikali na dini kupata matibabu yao kulingana na hadhi zao.

“Tunaweka utaratibu kwa viongozi kutokana na uzito wa majukumu yao, lakini nitumie fursa hii kuwakaribisha wana Dar es Salaam na Watanzania kwa jumla matibabu haya yatatolewa bure, waje kutibiwa na pale itakapotakiwa kupewa rufaa watatoa melekelezo madaktari wenyewe,” amesema.

Pia, amesema meli hiyo ina vifaa vya kufanya uchunguzi magonjwa ya moyo na upasuaji kwa kutumia teknolojia ya kisasa ikiwamo maroboti.

Akizungumzia ujio wa meli hiyo, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian amesema uhusiano mwema wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili ni sababu ya meli hiyo kuja nchini.

“China na Tanzania ni ndugu kama kaka na dada, hatuwezi kuachana ni uhusiano uliojengwa na viongozi wetu miaka mingi iliyopita. Hata kuwasili kwa meli hii ya kutoa matibabu bure kwa watu ni ushahidi tosha,”amesema.

Awali, Meja Jenerali Amri Salim Mwami amesema ujio wa meli hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Jeshi la Tanzania na miaka 60 ya urafiki kati ya Tanzania na Jeshi la Ukombozi la Watu wa China.

“Huduma zitakazotolewa na meli hii ni upasuaji, vyumba nane, CT Scan na vifaa vingine vinavyohitajika na nina imani maradhi yote ya kawaida yanaweza kupatiwa matibabu,” amesema.

Amesema katika meli hiyo kuna watu takribani 350 kati ya hao, 140 ni madaktari na wamegawanyika ikiwamo madaktari bingwa, madaktari wa kawaida, wauguzi na wafamasia.

“Katika kipindi cha siku tano watakachokuwa hapa, madaktari bingwa watajumuika na madaktari wa hapa nchini katika hospitali zetu kubwa ikiwamo Mloganzila, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Taifa ya Muhimbili pamoja na Taasisi ya Mifupa (Moi) watakuwa wanabadilishana uzoefu,” amesema.

Amesema madaktari wa kawaida watakuwa na sehemu yao ya kutoa huduma ikiwamo Mbagala Zakhem, Bunju Shule watafanya kazi kwa utaratibu utakao tangazwa baadae.

“Mbali na matibabu watakuwa na msaada wa kijamii watatembelea vituo vya yatima na kuona namna ya kuwasaidia kuwapa misaada,” amesema.

Related Posts