FAO WATOA DOZI MIL.3.9 ZA CHANJO YA SOTOKA YA MBUZI NA KONDOO

 -WOAH, AU-IBAR kuongeza takribani dozi Mil.6 nyingine

Shirika
la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) limeikabidhi Serikali ya
Tanzania dozi Mil. 3.9 za chanjo ya ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na
Kondoo kwenye hafla iliyofanyika leo Julai 16, 2024 wakati wa Ufunguzi
wa Warsha inayohusu Ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi kwenye eneo
la Afya ya wanyama jijini Arusha.

Akizungumza mara baada ya
kukabidhiwa chanjo hizo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof.
Riziki Shemdoe amelishukuru Shirika hilo kwa msaada huo ambapo
amebainisha kuwa hatua hiyo inaunga mkono mipango ya Serikali kupitia
Wizara yake kwa mwaka huu wa fedha ambapo imetenga takribani Shilingi
Bil. 28 kwa ajili ya kuendesha zoezi la chanjo ya mifugo nchi nzima.

Prof.Shemdoe
ametoa rai kwa Mashirika mengine ya kimataifa na wadau wa Sekta binafsi
kushirikiana na Serikali katika eneo la uboreshaji wa afya ya wanyama
ambapo amewaomba FAO kuongeza dozi nyingine za chanjo ili kukidhi idadi
ya wanyama waliopo.

“Lakini pia kipekee niwashukuru sana Shirika
la kimataifa la Afya ya wanyama (WOAH)  kwani nao wametuambia wapo
tayari kutoa zaidi ya dozi Mil.3 huku Shirika la Umoja wa Afrika
linaloshughulikia ustawi wa wanyama (AU-IBAR) wakikusudia kutupa zaidi
ya dozi Mil.2 kwa hiyo kwa haraka haraka unaweza kuona wadau wetu hawa
watakuwa wametupa takribani  dozi Mil.10” Ameongeza Prof. Shemdoe.

Kwa
upande wake Mwakilishi wa FAO Bi. Stela Kiambi ambaye ndiye
aliyekabidhi chanjo hizo amesema kuwa Shirika lake linatambua kuwa afya
bora ya wanyama inachangia afya bora ya binadamu hivyo Shirika lake
litaendelea kushirikiana na Wizara kwenye kampeni yake ya kutoa chanjo
ya wanyama nchini kote inayotarajia kuanza wakati wowote kuanzia sasa.

Naye
Mwakilishi wa kanda ya Afrika Mashariki kutoka  Shirika la kimataifa
linaloshughulikia afya ya Wanyama (WOAH) Dkt. Samuel Wakhusama amesema
kuwa Shirika lake limeandaa Warsha hiyo kwa kushirikiana na mashirika
mengine ili kujadili namna ya kutokomeza magonjwa ya Sotoka na Mbuzi na
Kondoo na ule wa kichaa cha Mbwa ifikapo mwaka 2030.

“Tunataka
nchi zetu zihakikishe  wanyama wanaouzwa wapo salama kiafya na wale
wanaonunua wanyama hao wawe na uhakika na usalama wao na ndio maana
tumekutana hapa ili kujadili kwa pamoja Serikali na Sekta binafsi  na
kupata suluhu ya kuangamiza magonjwa ya wanyama kwa njia rahisi”
Amesisitiza Dkt. Wakhusama.

Warsha hiyo ya kujadili Ushirikiano
wa Serikali na sekta binafsi kwenye eneo la Afya ya wanyama imeandaliwa
na  Shirika la kimataifa linaloshughulikia afya ya Wanyama (WOAH) na
inatarajiwa kuhitimishwa Julai 18, 2024 jijini Arusha.

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) Bi. Stela Kiambi (kulia) akimkabidhi Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe sehemu ya dozi milioni 3.9 za Chanjo ya Sotoka ya Mbuzi na Kondoo kando ya Mkutano wa Ushirikiano baina ya Serikali, Sekta binafsi na Umma kwenye eneo la huduma za wanyama unaofanyika Julai 16, 2024 jijini Arusha.

Related Posts