Mwanamke aliyekuwa mhudumu wa Grocery ya kuuza vinywaji Faraja Bembela mwenye umri wa miaka 28 mkazi wa kijiji cha Lusisi wilayani Wanging’ombe ameuawa na bosi wake ambaye jina limehifadhiwa kwa madai ya kusababisha hasara ya Sh.50,000.
Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe Mahamoud Banga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo kwa njia ya simu Julai 16, 2024, ambapo amesema marehemu ameuawa kwa kushambuliwa sehemu mbalimbali za mwili wake na mtu anayedaiwa kuwa bosi wake akishirikiana na kijana mwingine ambaye tayari amekamatwa.
Kamanda amesema marehemu alianza kushambuliwa akiwa ndani ya Grocery hiyo lakini baada ya kuona wamemuua wakamchukua na kwenda kumtupa katika misitu ya Tanwatt iliyopo wilayani humo.
Banga amesema tukio hilo limetokea Julai 14,2024 majira ya saa kumi alfajiri chanzo kikitajwa kuwa katika mahesabu wakati wa kukabidhiana na bosi wake kulionekana kuna hasara ya Sh. 50,000.
Kamanda Banga amewataka wananchi mkoani Njombe kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwani suala Sh.50,000 wangeweza kukubaliana na kukatana kwenye mshahara.