MWANASPOTI limepata taarifa za ndani kutoka KMC, kuhusiana na kiungo rasta, Awesu Awesu kuvunja mkataba wa miaka miwili na timu hiyo, kisha kusaini Simba ambayo imepiga kambini Misri kujiandaa na msimu ujao.
Kiongozi mmoja wa KMC, amebainisha kwamba Awesu alivunja mkataba wake kwa Shilingi 50 milioni, baada ya kuona ugumu wa kuondoka akiwa bado na mkataba, hivyo hakuwa na namna nyingine zaidi ya uamuzi alioufanya.
“Kabla ya Awesu kuvunja mkataba kulikuwepo makubaliano baina ya viongozi wa Simba na KMC, ikawa ngumu kuelewana kwa sababu mchezaji alikuwa na mkataba wa miaka miwili, hivyo isingekuwa rahisi kumuachia.
“Kwa sasa tumemalizana na Awesu ambaye tayari amesaini Simba miaka miwili, ametimiza ndoto yake kwani alitamani apate fursa ya timu inayocheza michuaono ya kimataifa.”
Mmoja wa viongozi wa Simba alikiri kumalizana na Awesu na kwamba muda wowote anaweza akajiunga na wenzake kambini nchini Misri.
“Ni mchezaji mzuri ana uzoefu kwani amezichezea timu mbalimbali hapa nchini ikiwemo Azam FC, hivyo tunaamini atakuwa na mchango katika timu yetu ambayo tumejipanga kufanya makubwa baada ya kukosa ubingwa kwa muda mrefu,” alisema.
Kutua kwa Awesu ndani ya Simba kunaifanya timu hiyo kufikisha wachezaji 13 wapya waliosajiliwa kuelekea msimu ujao wa 2024-2025.
Wengine ni Joshua Mutale, Steven Mukwala, Jean Charles Ahoua, Augustine Okejepha, Deborah Fernandes, Valentino Nouma na Karaboue Chamou, Yusuph Kagoma, Omary Abdallah Omary, Valentino Mashaka, Abdulrazack Mohamed Hamza na Kelvin Kijili.
Awesu atakuwa na kazi ya ziada kufanya ndani ya kikosi cha Simba hasa eneo la kiungo mshambuliaji anapocheza kwani anakutana na ushindani wa namba kutoka kwa Edwin Balua, Ladaki Chasambi, Omary Abdallah Omary, Joshua Mutale na Jean Charles Ahoua.