MCHEZAJI mkongwe wa timu ya taifa ya kikapu, Amin Mkosa amesema mfumo wa uendeshaji wa baadhi ya klabu nchini ndiyo unaofanya zikose udhamini.
Akizungumza na Mwanasposti juzi Dar es Salaam, Mkosa alisema mchezo huo umeshindwa kuendana na ukuaji wa kikapu duniani katika mfumo wa kibiashara unaoweza kuwa chanzo cha kipato kwa wachezaji kwa sababu timu zimekuwa zikiwategemea watu ili kucheza mashindano.
“Nchi zingine zimefanikiwa kutokana na kuwekeza katika promosheni na kuutangaza mchezo, kitu ambacho kinaleta hamasa na kukuza mchezo katika jamii,” alisema Mkosa.
Pia alisema kuna tatizo katika uendeshaji wa klabu ni tatizo kutokana na viongozi wengi kutokuwa na taaluma ya utawala wa mchezo inayosaidia katika ufanikishaji na uendelezaji michezo.
“Ni taaluma ambayo ni muhimu kwa viongozi wa michezo kuwa nayo, hivyo inawafanya (wengi waliopo) kutokuwa na uelewa wa jinsi gani wanaweza kuendesha timu kitaalamu,” alisema mchezaji huyo.
Akitoa mfano wa Uganda, Mkosa alisema nchi imewekeza nguvu katika udhamini wa timu na kila timu ina udhamini wake.
“Kila timu inakuwa na mdhamini wake ukiachana na udhamini wa ligi. Kwa hapa nchini tumeshindwa kufikia huko kutokana na mfumo wa uendeshaji,” alisema Mkosa aliyewahi kuchezea timu ya Betway Power katika Ligi ya Kikapu Uganda.
Akizungumzia Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), alisema msimu huu ni mgumu kutokana na timu zote kujipanga na kuwa na wachezaji wenye uwiano sawa kimchezo.
“Timu inaweza kushinda au kupoteza kwa yeyote. Hadi sasa katika mzunguko kwanza timu zote zimepoteza mchezo, hii inaonyesha ukomavu wa hali ya juu sana wa ligi yetu.”