Nape aomba radhi kwa kauli ya ‘ushindi nje ya boksi’

Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewaomba radhi wananchi na wapenda demokrasia nchini kutokana na kauli aliyoitoa kuwa si lazima CCM ishinde kura kwenye boksi, bali kuna njia nyingine zikiwemo alizosema za haramu.

Akizungumza kupitia video aliyorekodi, leo Jumatano Julai 17, 2024 Nape ameomba radhi wote walikerwa na kauli yake.

“Nimeuona mjadala kwenye mitandao, lakini kama nilivyosema kauli ile ilikuwa utani lakini naona umekuwa mjadala mrefu wakati huu kwa sababu tunaelekea katikia uchaguzi. Nawapa pole ambao wamesumbuliwa na kuteseka na huu mjadala, nawapa pole na naomba radhi, nasisitiza haikuwa serious,”amesema Nape.

Nape aliyewahi kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, alitoa kauli hiyo iliyoibua mjadala juzi Julai 15, 2024 usiku alipotembelea soko la Kashai mkoani Kagera na kuzungumza na wananchi.

Muktadha wa kauli hiyo ilikuwa ni kuwahakikishia ushindi wa Mbunge wa Bukoba Mjini, Stephen Byabato katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2025,

Mape ambaye kwa sasa ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema:

“Unajua nyie sikilizeni, matokeo ya kura sio lazima yawe ya kwenye boksi, inategemea nani anahesabu na kutangaza. Na kuna mbinu nyingi kuna halali, nusu halali na kuna haramu na zote zinaweza kutumika ilimradi tu mkishamaliza, unamwambia Mwenyezi Mungu nisamehe pale nilipokosea,” alisema.

Kauli hiyo ya Nape, ilipingwa jana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla ambaye alisema kauli hiyo haitokani na msimamo wa chama hicho.

“Kuna kiongozi nimemsikia huko mitandaoni anasema eti ushindi wa uchaguzi hautokani na kura za kwenye boksi, mimi nataka nimwambia hiyo kauli isitazamwe kuwa inatokana na CCM,” alisema Makalla.

Hii si mara ya kwanza kwa Nape kutoa kauli tata zenye kuzua mjadala katika kipindi cha kuelekea uchaguzi, hata Juni 2015, akiwa ziarani Sengerema alisema “CCM ingeshinda uchaguzi mwaka huo hata kwa bao la mkono.”

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts