Cheki wababe wa ngumi wanavyoviziana mikanda

BONDIA Oleksandr Usyk ndiye mwamba kwa sasa kwenye ngumi za uzito wa juu duniani (heavyweight), kufuatia kushinda na kushikilia mikanda minne ambayo ni WBC, WBA, WBO na IBF.

Mwamba huyo aliichukua mikanda hiyo mikononi mwa mabondia wa Uingereza, Anthony Joshua na Tyson Fury.

Awali, alianza kwa kumvua mikanda mitatu Joshua ‘AJ’ kwenye mapambano mawili mtawalia kabla ya mwaka huu kumvua Fury mkanda wa WBC na kumfanya kuwa mwamba wa kwanza  karne ya 21 kushika mikanda minne tena akiwa hajapigwa (undisputed) wala kutoka sare, akishinda mapambano yote 22 aliyowahi kupigana.

Ni katika pambano dhidi ya Fury lililompa sifa kubwa ya kuwa ‘undisputed’ kwa kushika mikanda minne, lakini pia ndilo linalokwenda kumfanya apoteze mikanda miwili kama mambo hayatabadilika, kwani tayari amelazimika kuuachia ule wa IBF kwenda kwa Daniel Dubois mwenye haki ya kuuwania (mandatory) na utaenda kuwaniwa pia na Joshua.

Dubois na Joshua wanakwenda kuugombea mkanda huo na endapo mmojawao atampiga mwenzake, Septemba, mwaka huu ikimaanisha kwamba mkanda huo haupo tena mkononi mwa Usyk na ili aurudishe anatakiwa kuuwania mwakani baada ya kupigana na Fury mwezi Desemba, huku pia akiwa kwenye uwezekano wa kupoteza mkanda wa WBO alionao mbele ya Joseph Parker.

Parker kwa sasa amepata nafasi ya kuwania mkanda huo kufuatia kumpiga Zhilei Zhang na anausaka mkanda huo mbele ya alionao ambaye ni Usyk anayetakiwa kusubiri uamuzi wa WBO ambao kama watapata mpinzani wa Parker, watamtaka Usyk autetee au auachie uwaniwe na Parker dhidi ya bondia mwingine.

Hapo ndipo kazi ilipo kwa Usyk, kwani tayari ameshasaini kukipiga na Fury kama walivyokubaliana mapambano mawili na watazipiga Desemba, huku Parker akisikilizia kuuchukua mkanda wa WBO dhidi ya mpinzani atakayepangiwa kama Usyk atachomoa kupigana naye ili kuutetea.

Related Posts