Chadema: Hatutasusia uchaguzi, tutapambana kuwatoa madarakani

Dar es Salaam. Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimehitimisha mikutano yake ya Operesheni +255 Katiba Mpya kwenye Kanda ya Kaskazini kwa kauli nzito na maelekezo kwa wanachama wake.

Jana, Chadema ilikuwa na mikutano mitatu jijini Arusha, ambapo wa kwanza ulifanyika eneo la Nasai kisha kuhitimisha mkutano mkubwa wa hadhara eneo la Muriet. Katika mkutano huo Mwenyekiti wa chama hicho,  Freeman Mbowe amesema hawatasusia uchaguzi mkuu ujao hata kama Serikali haitakuwa tayari kuwapatia Watanzania Katiba Mpya.

Amesema wataingia kwenye uchaguzi huo kwa lengo la kupata viongozi wenye nia ya dhati ya kusimamia haki na kuwakomboa Watanzania.

Mbowe amesema katika ziara walizozifanya kwenye  maeneo mbalimbali, wamebaini wananchi wanalia na umaskini huku viongozi waliopo madarakani wakiwa wamelala.

“Tunatakiwa kujipanga, haya mambo hayaji hivihivi hawa watu wanaiba kura, tunajua hawawezi kutoa Tume Huru ya Uchaguzi kwa sababu hawawezi kushinda katika uchaguzi unaoendeshwa na Tume Huru wamezoea haramu,” amedai Mbowe.

Amesema wananchi wanapaswa kuwa jasiri kwa kuwa wana uwezo wa kuiondoa Serikali ya CCM madarakani kwa kushinda kwa kutumia Katiba na Tume ya Taifa ya Uchaguzi iliyopo kwa sababu ushahidi ni kile walichokifanya mwaka 2015 na kupata majimbo mengi.

“Tulishinda kwa tume iliyopo sasa na Katiba hiihii, sasa kama hawatoi Katiba mnataka tususie uchaguzi (wananchi) au tupambane hivihivi. Hatuwezi kususia shamba la mahindi kwa nguruwe, wale hawa tutawakabili wanavyokuja na tunawahakikishia tutashinda na tuna uwezo huo,” amesema.

Katika mkutano huo, Mbowe amesema wananchi wa Kanda ya Kaskazini wanachohitaji warudishe silaha zao za kisiasa walizozitumia mwaka 2015, ambapo kwa Arusha walishinda majimbo sita kati ya saba, na Kilimanjaro katika majimbo tisa walishinda saba.

Amesema kila wanakopita wanarejesha chama hicho kwa wananchi ili wakitumie kumaliza umasikini uliotamalaki nchini huku akisema wanahitaji kuona kila mtu anakuwa wakala wa kupigana vita.

“Tunahitaji kila mwananchi ashiriki kupigana vita hii ili kila mtu aache kulalamika kwani, Chadema ni chama cha ukombozi kwa wananchi hatuwezi kuvumilia viongozi wanaishi maisha ya peponi halafu wananchi wanataabika na shida,” amesema.

Naye Mwenyekiti Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amesema kitendo cha Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kujivunia haramu ya kuiba kura ni kutishia usalama wa nchi.

“Waziri kutangaza utaiba kura katika uchaguzi unaokuja si jambo la kufumbia macho tusipokuwa wasela na majasiri wa kupigania haki zetu ikiwemo kuingia barabarani hawa jamaa watatuona wajinga,” amesema.

Hata hivyo, Nape jana ameandika kwenye ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, akisema kauli hiyo imekuzwa na kwamba alikuwa kwenye lugha za utani na kuwa yeye ni muumini wa demokrasia.

Tayari, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, naye amesema kauli ya Nape haitokani na msimamo wa chama hicho.

“Kuna kiongozi nimemsikia huko mitandaoni anasema eti ushindi wa uchaguzi hautokani na kura za kwenye boksi, nataka nimwambie hiyo kauli isitazamwe kuwa inatokana na CCM,” amesema Makalla. 

Lema katika maelezo yake amedai kabla ya kutoa kauli hiyo alipaswa kujitathimini kwa kutambua kuwa ni kiongozi anayeshika nafasi ya uwaziri hivyo hawezi kujivunia kuiba kura.

“Maneno haya wanasema kwa sababu wananchi tunahofu, tungekuwa tunajihamini tungeingia barabarani kesho tuseme Nape atoke ofisini, huyu mtu anatishia usalama wa nchi,” amesema Lema.

Katika hatua nyingine Lema amewatangazia wananchi hao mkutano huo unahitimisha mzunguko wa majimbo yote 35 yaliyopo katika kanda hiyo wakifanya jumla ya mikutano 166.

“Baada ya hapa tutapumzika wiki moja na kuingia Kanda ya Kati Dodoma, Morogoro na Singida niwahakikishie tumezunguka majimbo yote 35 ya Kaskazini tumefanya ukutano kwa asilimia 50 kila kata,”amesema.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts