Mchungaji Odero aonya wahubiri wanaozuia watu kutibiwa hospitali

Mwanza. Muhubiri maarufu wa Kenya, Ezekiel Odero, amewapinga baadhi ya manabii wanaozuia wagonjwa kutumia dawa na huduma za hospitali ili wapate miujiza na uponyaji kutoka kwao, huku akiwataka watumishi hao wahubiri neno la Mungu bila kupotosha.

Mchungaji Odero ametoa kauli hiyo leo Jumatano Julai 17, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza.

Amesema katika maandiko matakatifu hakuna mahali Yesu amekataza matibabu, hivyo haungi mkono kauli za baadhi ya wanaojiita watumishi wa Mungu na manabii wanaokataza wajawazito kujifungulia hospitali, ama wagonjwa kutoroka hospitali na kuacha dawa ili wapate miujiza ya uponyaji.

“Mungu alimuumba daktari na akamsomesha, daktari si mchawi, mambo ya matibabu ni muhimu sana, watoto wangu wamezaliwa hospitali na mke akafanyiwa upasuaji, inamaanisha madaktari wamenisaidia sana. Hakuna mahali Yesu amesema tukatae matibabu, kwa hiyo simuungi mkono mtu yeyote anayezuia watu kwenda hospitalini.”

“Katika huduma yetu hii tuko na madaktari ambao wanatusaidia kukagua, kanisani kwetu kuna madaktari tunatambua huduma ya madaktari na huwa tunapokea wagonjwa wenye ruhusa ya hospitali na Serikali na hatumwambii mtu aache dawa alizopewa hospitali,” amesema mchungaji huyo.

Wakati huo huo, Mchungaji Odero ametoa wito kwa viongozi wa dini kujiweka kando na siasa.

Amesema wao wametumwa kuhubiri neno la Mungu na siasa na dini haziambatani, huku akiwasihi kutoa maoni yao kwa wanasiasa kwa njia ya heshima ili kutowavunjia heshima yao.

Mchungaji huyo ambaye yupo jijini Mwanza, atafanya mkutano wa siku tano wa miujiza na ishara kuanzia Julai 24 hadi 28, mwaka huu katika Uwanja wa CCM Kirumba.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akizungumza baada ya kumpokea muhubiri huyo, amesema Taifa linahitaji maombi ili kupiga hatua na kila mtumishi wa Mungu anaheshimiwa kwa uwezo wake, huku akisisitiza mkutano huo wa injili ni fursa ya kiuchumi kwa wakazi wa Mwanza.

“Nchi yetu bila maombi haiwezi kwenda, tunaamini katika maombi na sala, siku zote watumishi wa Mungu ni watu ambao tunawapa ushirikiano mkubwa. Sisi tunaheshimu kila mtu na mafuta yake (upako), kazi anayofanya mtumishi wa Mungu mimi nikilazimisha sitaiweza,” amesema Mtanda.

Marry Edward aliyetoka Arusha kuja Jijini Mwanza kwa ajili ya mkutano huo, amesema; “Pasta Ezekiel yuko vizuri, sisi ni mashuhuda yeye hakuzuii kutumia huduma ama dawa ulizoandikiwa hospitalini. Natarajia watu kufunguliwa sana kwa sababu tumeshuhudia sehemu mbalimbali akifanya hivyo.”

Naye, Revinson Revelian ambaye ni Mhasibu wa Umoja wa waendesha bodaboda Mkoa wa Mwanza, amesema wamefika kumpokea mhubiri huyo na kupata maombi yake ili kukomesha changamoto mbalimbali wanazokutana nazo ikiwemo ajali, vifo na matukio mengine mabaya barabarani.

Aprili 27, 2023 Polisi nchini Kenya katika Kaunti ya Kilifi walimkamata mchungaji Odero kwa tuhuma za kuhusika na vifo vya waumini katika Kanisa lake linalojulikana New Prayer Centre.

Tukio hilo lilitokea katika Kaunti ya Kilifi siku chache tangu kuibuliwa mauaji ya waumini wa kanisa lililokuwa linaongozwa na Mchungaji Paul Mackenzie.

Related Posts