Nabi amtaka Mayele, amuita Kaizer Chiefs

Kocha mpya wa Kaizer Chiefs, Nasreddine Nabi ameuomba uongozi wake kuhakikisha unamsajili mshambuliaji wa Pyramids FC, Fiston Mayele kwa ajili ya kuimarisha safu yao ya ushambuliaji.

Mtandao wa Kingfut wa Misri umefichua kuwa miongoni mwa mapendekezo ya mwanzo ambayo Nabi ameupa uongozi wake muda mfupi baada ya kujiunga na timu hiyo ni kuhakikisha Mayele anaichezea timu hiyo msimu ujao.

Kiwango bora ambacho Mayele anakionyesha kwenye Ligi Kuu ya Misri lakini pia ufahamu ambao Nabi anao kwa Mayele kutokana na kuwahi kufanya naye kazi walipokuwa Yanga zinaonekana kuwa sababu ambazo zimemfanya kocha huyo atamani kufanya tena kazi na mshambuliaji huyo raia wa DR Congo.

Mayele amekuwa moto wa kuotea mbali katika Ligi Kuu ya Misri msimu huu ambapo hadi sasa anaongoza chati ya kufumania nyavu akiwa amefunga mabao 14.

Lakini pia mshambuliaji huyo amepiga pasi tano za mwisho na hivyo kuchangia kuifanya timu yake kuongoza msimamo wa ligi kuu ya Misri.

Hata hivyo kikwazo kwa Kaizer Chiefs kinaonekana kitakuwa ni fedha ambazo Pyramids itahitaji ili kumuachia mshambuliaji huyo.

Ikumbukwe Mayele alinunuliwa na klabu hiyo ya Misri mwaka jana kwa dau la Dola 800,000.
 

Related Posts