Tetemeko la ardhi lilivyozua taharuki Moshi

Moshi. Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa ‘Ritcher’ 4.6 lililopita usiku wa Julai 16, 2024, likitokea Nairobi, Kenya na kuzua taharuki kwa wakazi wa Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Hata hivyo inaelezwa kuwa mbali ya kuzua taharuki, tetemeko hilo halijasababisha madhara.

Kwa mujibu wa Mjiolojia Mwandamizi kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania, Gabriel Mbogoni, tetemeko hilo lilitokea saa 2:32 usiku jana likitokea nchi jirani ya Kenya.

Akizungumzia kutokea kwa tetemeko hilo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Zephania Sumaye amesema hakuna madhara yaliyoripotiwa kuhusiana na tetemeko hilo.

“Mpaka sasa hakuna madhara yoyote ambayo yameripotiwa kuhusiana na tetemeko hilo la ardhi,” amesema Sumaye.

Wakizungumzia taharuki ya tetemeko hilo leo Jumatano Julai 17, 2024, baadhi ya wananchi wa Moshi wamesema walipata mshituko baada ya kuona viti walivyokuwa wamekalia vikisogea.

Jenrose Makashi, mmoja wa wakazi wa Kata ya Msaranga, wilayani Moshi, amesema alishangaa kuona mtikisiko mkubwa umepita kwenye nyumba yao huku baadhi ya vitu kama meza na viti vikisogea.

“Jana jioni tulikuwa tumekaa, tunakula chakula cha jioni nyumbani, tulishangaa ghafla kuona mtetemo mkubwa. Tulifikiri tunanyanyuliwa kwenye viti tulivyokuwa tumekaa. Tulipata mshituko tukafikiri nyumba inaanguka,” amesema Makashi.

Naye Joseph Matei, mmoja wa wananchi wanaoishi Moshi Mjini amesema wakati tetemeko hilo linapita alikuwa amelala akashituka baada ya kusikia kishindo kikubwa kwenye nyumba yao, hali ambayo iliwapa hofu yeye na familia yake.

“Nilikuwa nimelala ghafla nikasikia kama kitanda kinatikiswa, sikujua ni nini. Baadaye nikasikia wenzangu wakisema ilikuwa ni tetemeko la ardhi,” amesema Matei.

Akinukuliwa siku za hivi karibuni, Mjiolojia Mbogoni alisema matetemeko hayo ya ardhi ambayo hujitokeza mara kwa mara maeneo ya Mkoa wa Kilimanjaro huwa yanapita kutokea  maeneo ambayo yako ukanda wa bonde la ufa na kwa kuwa Mkoa wa Kilimanjaro ni miongoni mwa maeneo hayo, ndiyo maana hupita mara kwa mara.

Amesema chanzo chake kinatokana na nguvu za asili ambazo zimejikusanya kwa miaka mingi na  Kilimanjaro iko jirani na mlima wa Oldonyo Lengai ambao huwa unalipuka mara kwa mara.

“Kipande hiki cha ardhi kinajaribu kujigawa kutoka bara la Afrika kuingia baharini, kwa hiyo nguvu ambazo ziligawanya mabara saba duniani, ndiyo yanayoendelea hadi sasa, ndiyo maana Afrika kuna ukanda wa bonde la ufa la Afrika Mashariki ambalo kwa sasa linataka kutenga hiki kipande cha Afrika kiingie baharini,” amesema Mbogoni.

Related Posts