DR Congo. Zaidi ya watu 70 wakiwemo wanajeshi tisa wameuawa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Congo baada ya watu wenye silaha kushambulia Kijiji cha Kinsele kilichopo kilomita 100 kutoka Mji Mkuu Kinshansa.
Mauaji hayo yalitokea Jumamosi Julai 15, 2024 huku miundombinu mibovu ikitajwa na Mbunge wa Jimbo la Kwamouth, David Bisaka kuwa chanzo cha taarifa hiyo kuchelewa kuripotiwa.
Kwa mujibu wa tovuti ya African news, Kijiji hicho kilichopo Jimbo la Kwamouth, kwa muda wa miaka miwili kipo katika mzozo kati ya jamii mbili za wenyeji ambazo ni: Teke na Yaka ambao umesababisha vifo vya mamia ya raia.
Kwa mujibu wa Bisaka akihojiwa na Shirika la habari la AP amedai kuwa washambuliaji walikuwa wanachama wa wanamgambo wa Mobondo, kikundi kinachodaiwa kutetea jamii ya Yaka.
“Kufikia leo asubuhi (Jumatatu, Julai 15), miili 72 tayari imepatikana na msako unaendelea kuitafuta zaidi msituni,” amesema Bisaka.
Aidha, Mwenyekiti wa Kijiji cha jirani, akiongea na Radio Okapi inayomilikiwa na Umoja wa Mataifa amesema ulinzi umeimarishwa katika vijiji hivyo huku miili mingine kitafutwa.
Shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch katika chapisho lake limesema mgogoro huo kati ya jamii hizo mbili ulianza tangu Juni 2022.
Licha ya usitishaji mapigano uliofanyika Aprili 2024 mbele ya Rais wa nchi hiyo, Félix Tshisekedi, mapigano kati ya jumuiya hizo mbili yameendelea na hata kuzidi katika wiki za hivi karibuni, bila jeshi la Congo kusimamia kutuliza ghasia hizo.