NI vita ya kisasi kati ya Ally Isanzu anayeongoza mbio za ubingwa wa Lina PG Tour na vijana watatu kutoka Arusha; Jay Nathwani, Garv Chadhar na Aliabas Kermali walioichafua rekodi yake ya kutoshindwa katika viwanja vya Arusha Gymkhana.
Isanzu anapambana tena na vijana hao katika mashindano ya wazi yajulikanayo kama Arusha Open ambayo yanaanza katika Klabu ya Gymkhana jijini humo kesho.
“Niko tayari kwa mashindano haya baada ya kufanya zoezi la kutosha katika viwanja vya TPC mkoani Kilimanjaro. Nataka kujiuliza wapi niliteleza mpaka nikaangukia nafasi ya tano baada ya kuongoza katika siku zote tatu kabla ya kuharibu ya mwisho,” alisema Isanzu na kuahidi kurekebisha makosa katika mashindano hayo.
Arusha Open ni mashindano ya wazi ya siku tatu na yanatarajiwa kuanza kesho na kumalizika Jumapili, Julai 21, mwaka huu ambapo mashimo 54 yatachezwa, kwa mujibu wa waandaaji.
Vita ya kisasi kati ya Isanzu na vijana hao siyo kivutio pekee cha mashindano ya mwaka huu ya Arusha Open, pia ipo ya wanawake itakayoongozwa na nyota wa timu ya taifa, Madina Iddi.
Kwa mujibu wa orodha ya washiriki iliyotolewa na Arusha Gymkhana, Madina atakuwa akikabiliana na upinzani mkali kutoka kwa Aalia Somji, Neema Olomi na Vicky Elias kutoka Dar es Salaam ambaye amebaki Arusha kwa ajili ya mashindano.
“Sikufanya vizuri sana katika mashindano ya Lina PG Tour. Kwa hiyo nimejinoa vya kutosha ili nifanye vizuri katika mashindano ya Arusha Open,” alisema Vicky ambaye pia ni mmoja wa wachezaji wa timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania.
Mchezaji mwingine wa kuangaliwa zaidi katika mashinadano yanayoanza kesho ni Neema Olomi kutoka Arusha ambaye rekodi yake ya ubora aliiweka nchini Uganda baada ya kushinda Uganda Ladies Open mwaka 2022.