Mfanyakazi wa shule akutwa amekufa kwenye tanki la maji

Arusha. Watu wawili wamefariki dunia jijini hapa akiwemo mfanyakazi wa Shule ya Msingi Shinda, Deogratius Shayo (50), ambaye mwili wake umekutwa ndani ya tanki la maji lenye ujazo wa lita 10,000.

Katika tukio lingine, mfanyabiashara wa pombe kali aliyejulikana kwa jina moja la Neema (40 – 45) pia amekutwa amekufa ndani ya nyumba yake, ikidaiwa kifo hicho kimesababishwa na matumizi makubwa ya pombe kali.

Akithibitisha kutokea kwa matukio hayo, leo Julai 17, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amesema mpaka sasa hakuna watu wanaoshikiliwa kutokana na vifo hivyo hayo.

“Matukio hayo yametokea jana Julai 16, 2024, na hadi sasa upelelezi unaendelea ikiwemo wa huyo mfanyakazi wa Shule ya Shinda, lakini kwa taarifa za awali inaonekana alijirusha mwenyewe kwenye tanki hilo,” amedai Masejo.

Amesema miili yote miwili imehifadhiwa Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru.

Akizungumzia tukio la mfanyakazi wake kufia kwenye tanki la maji, Mkurugenzi wa Shule ya Shinda, Hosiana Kimaro amesema mara ya mwisho alionana naye Jumatatu Julai 15, 2024, saa mbili usiku alipotoka shule kuelekea nyumbani kwake.

“Asubuhi nilipokuja sikumkuta kama nilivyozoea kumwona akifanya usafi au kupima vyakula vya kupika siku hiyo. Hata hivyo, sikutilia maanani sana nikidhani labda yupo eneo lingine au ametoka kidogo,” amesema Kimaro.

Hata hivyo, amesema baada ya muda kupita, alipata taarifa kutoka kwa wafanyakazi wengine wa shuleni hapo kuwa Deo haonekani na mkewe pia anamtafuta na simu ameiacha stoo.

“Ndio tukashituka na kuanza kumtafuta kabla ya kugundua moja ya tanki la maji liko wazi na mfuniko uko chini. Tulipochungulia tukamuona,” amesema mkurugenzi huyo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Long’dong, Kata ya Sokon One, Ibrahimu Nkurunzi amesema bado hawajajua chanzo cha mfanyakazi huyo kutumbukia kwenye tanki hilo la maji na kufariki dunia.

“Inadaiwa huyu jamaa hivi karibuni alikuwa na ugomvi na mwanamke wake juu ya malezi ya mtoto na jana alionekana kuhangaika, hivyo nadhani ni msongo wa mawazo umepelekea kujitumbukiza kwenye tanki lenye maji mengi ili ajidhuru,” amedai mwenyekiti huyo.

Hata hivyo, amewataka wananchi wake kuacha kujidhuru kwa lengo la kukabiliana na msongo wa mawazo.

“Kila mtu duniani hapa ana matatizo yake ingawa yanazidiana, lakini suluhisho sio kujiua bali tafuta mtu unayemwamini mueleze matatizo yako ili yapungue kichwani sio kunyamaza nayo mwisho unachukua hatua isiyofaa,” amesema mwenyekiti huyo.

Katika tukio lingine, mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Neema mwenye umri kati ya miaka 40-45 naye amekutwa amefariki ndani ya nyumba yake huku chanzo kikidaiwa ni matumizi makubwa ya pombe kali.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Lolovono, Kata ya Sokon One, Orgenes Lema amesema alipigiwa simu jana Jumanne Julai 16, 2024, asubuhi kuwa kuna mwananchi wake amekufa ndani ya nyumba yake.

“Nilipofika eneo la tukio, nilimkuta huyo mama maarufu sana hapa mtaani kwa jina la ‘Kirikuu’ akiwa amelala kitandani na amefunikwa. Nilimkagua na kupiga simu Polisi. Walipokuja walibaini ni kweli amefariki na wakachukua maiti yake kwenda kuihifadhi mochwari,” amesema Lema.

Amesema mwanamke huyo kabla ya mauti kumkuta, alikuwa akifanya biashara ya pombe na nyama ya nguruwe maarufu kitimoto, lakini licha ya kuwa alikuwa akiishi kwenye mtaa anaouongoza, hajui anatokea wapi wala ndugu na jamaa zake.

“Hapa tunahangaika kutafuta ndugu au jamaa zake maana alikuwa anaishi kwa mwanaume mmoja ambaye naye ni mnywaji tu na wamepatana barabarani wakaishi wote bila kufahamu ndugu zake,” amesema mwenyekiti huyo.

Balozi wa Mtaa wa Mnarani, Lazaro Laizer amesema mwanamke huyo alikatazwa na madaktari kunywa pombe baada ya hivi karibuni kulazwa hospitali kutokana na kuzidiwa na ulevi hadi kupoteza fahamu.

“Alishakatazwa maana alidhoofika sana, na hata wiki mbili zilizopita alikuwa na hali mbaya baada ya kutumia pombe hizi kali, lakini alisuguliwa na maji ya limao na chumvi kwenye nyayo, pia kunyweshwa maji baridi yaliyokorogwa na unga akapona na alikatazwa asinywe tena. Sasa nashangaa amekunywaje tena,” amesema huku akishangaa Laizer.

Related Posts