Rekodi kali za kuruka zinazosubiri kuvunjwa Olimpiki

WANAMICHEZO 10,500 watakuwa katika Jiji la Paris, Ufaransa kwa ajili ya michezo ya Olimpiki itakayofanyika kuanzia Julai 26 hadi Agosti 11, mwaka huu.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano hayo makubwa ya michezo duniani washiriki kutoka zaidi ya nchi 200 watakuwa nusu wanaume na nusu wanawake ambao watashindana katika michezo 32.

Kwa kawaida vivutio vikubwa katika mashindano hayo yanayofanyka kila baada ya miaka minne huwa ni kandanda, riadha na ndondi. Miongoni mwa mambo yanayosubiriwa kwa hamu katika riadha ni kuona baadhi ya rekodi ambazo zimedumu muda mrefu zinavunjwa.

Siku za nyuma ilikuwa ni kawaida kusikia rekodi moja au mbili za dunia zimevunjwa, lakini siku hizi ni tabu  kutokea. Sababu kubwa sio kwamba wanamichezo hivi sasa hawana uwezo na ujuzi mkubwa, bali ni kutokana na rekodi zilizopo zimefikia kilele au kukaribia uwezo wa juu wa mwili wa binadamu.

Matokeo yake ni kwamba zipo rekodi zilizodumu muda mrefu na kwa sasa hakuna dalili za kutokea mtu, sio tu kuzifikia bali kuzivunja. Moja ya sababu ya kutosikia rekodi zinavunjwa kirahisi ni kutokuwepo mwanya wa mwanamichezo kutumia dawa za kuongeza nguvu ili kupata mafanikio mazuri.

Miongoni mwa rekodi za dunia zilizodumu muda mrefu ni ile ya kuruka (high jump) upande wa wanawake iliyodumu miaka 37 iliyowekwa na mwanadada wa Bulgaria, Stefka Kostadinova 1987.

Rekodi hiyo ilivunjwa wiki mbili zilizopita, Julai 7, mwaka huu na binti wa Ukraine, Yaroslava Mahuchikh kwa kuruka mita 2.10 (futi 6.88).

Stefka atakuwepo Paris kshuhudia mwanamke aliyevunja rekodi kwa vile ni kiongozi wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) na ni rais wa Kamati ya Olimpiki ya Bulgaria.

Tangu 1987 hadi wiki mbili zilizopita wanawake wa nchi mbalimbali wamejitahidi kuivunja rekodi hiyo, lakini matumaini yamepotea hewani. Mchezo wa kuruka unasemekana ulianza kuchezwa Scotland katika karne ya 19.

Mtu wa kwanza kuruka urefu wa futi 7 (mita 2.13) alikuwa Charles Dumas wa Marekani mwaka 1956 na kufuatiwa na rekodi yake kuvunjwa na John Thomas wa Marekani mita 2.23  (futi 7 na inchi 33) mwaka 1960.

Dumas alifariki dunia 2003 baada ya kuugua ugonjwa wa saratani kwa karibu miaka 10. Baadaye rekodi hiyo  ilishikiliwa na Valeriy Brumel wa Urusi kwa miaka minne kwa kuruka mita 2.28 (futi 7 na inchi 53) mwaka 1964. Alifariki dunia 2003 akiwa na miaka 40.

Baada ya hapo alichomoza Vladimir Yashchenko wa Ukraine (wakati ule ikiwa sehemu ya Shirikisho la Kisovieti la  Urusi) ambaye aliruka mita 2.33 (futi 7 na inchi 71) mwaka 1977 na baadaye mita 2.35 (futi 7 na inchi  81) mwaka 1978.

Yaschenko alitawaliwa na pombe katika miaka ya mwisho wa maisha yake na kuiaga dunia 1999 akiwa na umri wa miaka 40. Kwa kawaida wanariadha wazuri hutumia kati ya hatua 12 na 14 kabla ya kuruka.

Hivi sasa ni miaka 25 tangu Javier Sotomayor alipoweka ile rekodi ya kuruka futi 8 katika mashindano yaliyofanyika Budapest, Hungary na suala linaloulizwa na wengi ni je ipo siku rekodi hiyo itavunjwa?

Sotomayor alichomoza kuwa mrukaji mzuri tangu alipokuwa na umri wa miaka 15 aliporuka urefu wa mita 2 na kuushangaza ulimwengu. Aliweka rekodi ya kwanza ya dunia 1984 na kuivunja miaka minne baadaye kwa kuruka mita 2.43 (futi 7 na inchi 11) katika mashindano yaliyofanyika katika mji wa Salamanca, Hispania.

Julai 29, 1989 katika mashindano ya nchi za Amerika ya Kati na Caribbean yaliyofanyika San Juan, Puerto Rico.

Sotomayor aliweka rekodi hiyo mpya ya dunia ya urefu wa mita 2.44 na kuwa mtu wa kwanza katika historia kuruka urefu wa futi 8.

Baadaye Julai 27, 1993 kule Salamanca, Hispania alifanya maajabu ambayo hayakutarajiwa kutoka katika mwili wa binadamu kwa kuruka urefu wa zaidi ya futi 8, rekodi ambayo imebaki hadi leo.

Nyota huyo aliendelea kuruka mashindano mbalimbali hadi  2000 katika michezo ya Olimpiki iliyofanyika Sydney, Australia. Sotomayor hivi sasa ni mshauri wa michezo wa Kamati ya Olimpiki ya Cuba.

Hivi karibuni Sotomayor alisema akitokea mtu kuweza kuvunja rekodi yake kuruka ni vizuri afanyiwe uchunguzi kama alitumia dawa za kuongeza nguvu mwilini au alivaa mbawa bandia za mwewe.

Lakini kwa hivi sasa rekodi ya Sotomoyor ni kiboko na labda waachiwe mwewe na kunguru kuivunja. Michezo ya Olimpiki ndio inakaribia. Suala ni je atatokea mwewe wa kuivunja hiyo rekodi? Tusubiri mashindano ya Paris yatatupa jibu.

Related Posts