Heri ya uzee wa kina Chama, kuliko ubishoo wa wazawa!

NI kweli tunadanganywa. Na tunajua kabisa tunadanganywa na nyota wa kigeni wanaokuja kucheza soka la kulipwa hapa nchini. Tunajua wengi huwa na umri mkubwa zaidi ya ule uliopo katika pasipoti zao. Lakini tunamezea kwa vile hata wachezaji wazawa nao kamba nyingi.

Wazawa nao wanatudanganya sana kwa kufeki umri. Kibaya zaidi, kuna baadhi ya wachezaji wanasaidiwa na mamlaka za soka kufoji umri huo. Inafanywa hivyo, ili wazitumikie timu za taifa, kuanzia zile za vijana hadi za wakubwa. Mtabisha nini wakati sakata la Nurdin Bakar na mkasa wa Tanzanite mwaka 2004 bado unaishi. Baadhi ya wachezaji ni wadogo zetu. Watoto zetu, wanazaliwa na tunaona, lakini ghafla unashangaa kusikia wamedogoshwa.

Achana na hao wazawa, hata wageni wanaokuja kukipiga hapa nchini wanafoji sana umri. Ndio maana ilikuwa vigumu kuamini eti, Meddie Kagere wakati anakuja kwa mara ya kwanza alikuwa na umri wa miaka 32. Akili ilikuwa haikubali. Sio kwa sababu ya muonekano wake, lakini hata rekodi zake za uchezaji zinamkana. Pia ilikuwa vigumu kuamini Emmanuel Okwi alikuwa ni mdogo kwa John Bocco au utakubali vipi kirahisi eti, Amissi Tambwe alikuja akiwa na umri wa miaka 24. Kumbuka hiyo ilikuwa mwaka 2013.

 Kwa sasa nyota huyo wa zamani wa Vital’O, Simba na Yanga ana umri wa miaka 35. Ilikuwa hivyo hivyo kwa Joash Onyango.

 Hadi leo hakuna anayeamini kama Onyango ana umri wa miaka 31, yaani analingana na Jonas Mkude!

Udanganyifu huu kama nilivyoeleza haupo kwa wageni tu, hata baadhi ya nyota wetu wanatupiga fiksi sana kwa kujifanya viserengeti boys, ilihali ni vibabu. Wengi wanaotudanganya tunawajua!

Bahati mbaya kasumba hii ya udanganyifu kwa nchi za Afrika, haupo kwa wanasoka tu, bali hata mastaa wa muziki, filamu na urembo wana tatizo hilo.

Wanawadanganya sana mashabiki wao kwa kujifanya vitoto vidogo, ilihali wengi wao wamekula chumvi za kutosha. Wanasahau utotoni mitaani walicheza na watoto wenzao.

Wameishi ndani ya jamii, hivyo inayowajua kuliko wanavyojijua wenyewe.

Ni bahati tu, katika fani nyingine sio rahisi kubaini udanganyifu tofauti na ilivyo kwenye soka. Katika soka hata mchezaji ajishushe umri vipi ataumbuliwa na utendaji kazi wa mwili wake uwanjani.

Si mnakumbuka alivyoumbuka JJ Okocha aliyestaafu soka ikijidai ana umri wa miaka 29.

Nani hajui umri huo ndio huwa kilele cha mafanikio ya mchezaji na kwa soka alilokuwa akilipiga Okocha ni vigumu kuamini alistaafu akiwa na umri huo tena hiari bila ya kuwa majeruhi!

Kina Okocha wapo wengi ndani na nje ya nchi na angalau wachezao nafasi ya ukipa, wanamudu kuendelea kucheza kuliko nafasi nyingine hasa kiungo au ushambuliaji zinazohitaji pumzi za kutosha.

Lakini unaweza kusema ni afadhali kuwa na wachezaji wazee kama kina Kagere na Clatous Chama au Onyango wanaozitumikia nafasi zao kwa ufanisi kuliko kuwa na vijana goigoi na wasio na faida kwa timu.

Kwa jinsi wachezaji wetu vijana wanavyoshindwa kufanya kazi uwanjani, unaona ni bora wahenga kutoka nje ya nchi waendelee kuja kutudanganya tu. Na bora kuendelea kuwakumbatia nyota wa kigeni katika klabu zetu.

Iangalie kazi anayoifanya Khalid Aucho ama Chama, kisha linganisha na ile ya kina Ibrahim Ajibu, Said Ndemla na wengine vijana wa Kitanzania ndio utajua namaanisha nini?

Kwa nini kina Elvis Rupia, Kagere, Chama, Aucho na wageni wengine wasiendelee kula mishahara minono nchini, iwapo kila uchao wanajua kuwapa raha mashabiki wa klabu hizo?

Nimeshangaa kuibuliwa tena mjadala wa idadi wa wachezaji wa kigeni ipunguzwe kutoka 12 iliyopo hadi iwe nane na ikiwezekana watano. Kisa, eti wanawabania wazawa. Wazawa hao wanaoshinda Instagram na katika pati za usiku wakiserebuka na kusahau majukumu yao uwanjani?

Yeyote mwenye wazo na anayeamini wageni wanawabania wazawa anastahili kupimwa afya ya akili, kwani leo tunajitamba kufika fainali za CAF, kushiriki fainali za Afcon mara kadhaa mfululizo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na wachezaji wa kigeni. Wamesaidia kuwamsha na kuwachangamsha wazawa waliobweteka na kukalia uvivu. Kadri wachezaji wazawa wanavyopata changamoto kubwa katika klabu zao ndivyo upeo na ushindani wao unaongezeka na kulisaidia taifa. Wageni huwaamsha kutoka usingizini na wengine kujifunza.

Utabisha nini wakati Simba imefika robo fainali mfululizo ya michuano ya kimataifa kwa sababu na kina Kagere, Okwi na wakongwe wengine wa kigeni waliochangamana na wakongwe wa Kibongo kama Bocco, Kapombe huku mayanki wakisinzia kwenye mabenchi na kufurahia mishahara ya bure.

Yanga imecheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza ikiwa wachezaji wengi wa kigeni waliojituma na kuwafanya wazawa nao kuamka na kupambana kiume kuibeba timu na kuamka kwao kumefanya Stars kwenda fainali za Afcon 2019 na 2023 na kucheza Chan 2022.

Ndio maana sikushangaa kusikia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye kitaaluma ni kocha wa soka, kupotezea hoja ya kupunguzwa kwa idadi ya wageni. Nimefurahi kusikia hata Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia naye akiwananga wazawa kwa uvivu.

Hatuwezi kuwabania wageni wanaoifanya Ligi yetu kuwa katika 10 Bora kwa sababu ya kutaka kuwafurahisha wachezaji wasiotaka kuamka na kutambua soka ni maisha yao. Usimwamshe aliyelala usije ukalala wewee…!

Hizi kejeli za kuwaita kina Chama kuwa eti ni wahenga, vibabu na wazee ni kujivunjia heshima na wivu wa kufikiria tu, ila ukweli kiuhalisia jamaa hao ni wazee wa kazi na wana faida kuliko vijana mabishoo na mizigo!

Naamini kama wachezaji wazawa na hasa vijana wangekuwa wakiifanya kazi yao kwa ufanisi na kuzibeba timu, viongozi wasingepoteza muda kubeba wachezaji wakongwe kutoka nje ya nchi. Wasingeshindana kuleta mapro wazee kutoka nje ya nchi na pengine mamilioni ya fedha wanayolipwa wageni hao wangemwagiwa wao na kuneemeka.

Nadhani imefika wakati wachezaji vijana nchini kuchangamka na kutumia vipaji vyao kuweza kujitengenezea jina na kujiuza badala ya kuendelea kulalamika kubaniwa na maproo wa kigeni. Kisha wakajitokeza wachache kuwaunga mkono na kuwapigania kwa kutka idadi ya wageni ipunguzwe ili wazawa wapate nafasi.

Kusema kuwa wageni wanachangia kushusha soka la Tanzania na hasa Taifa Stars ni kujidanganya tu. Bahati nzuri namba hazijawahi kudanganya hata siku moja. Tupige hesabu ndogo tu.

Ligi Kuu inashirikisha klabu 16 ambazo wastani wao wa kusajili kikosi kizima huwa si chini ya wachezaji 25 na haizidi 30, ukiacha wale vijana wa U20 wanaobebwa na kanuni za ligi hiyo.

Kanuni ya usajili kwa wachezaji wa kigeni ni wasiozidi 12 na sio klabu zote zinamudu idadi hiyo, kutokana na nyota hao wa kigeni kuwa na gharama katika kuwamiliki ikiwamo kuwalipa vibali vya kuishi, vibali vya kazi na mishahara wanayolipwa kwa dola.

Ukiondoa Simba, Yanga, Azam na sasa Singida Black Stars zinazomudu kubeba wachezaji wote 12, wengine kama Coastal Union, Kagera Sugar, Namungo, Tabora United, Pamba na nyingine huwa hazifikishi idadi hiyo. Na hata kama klabu zote 16 zingekuwa zimemudu kusajili wachezaji 12 kila moja maana yake idadi ya wageni ingekuwa na wachezaji kama 192 tu. Wengine zaidi ya 250 wakiwa ni wazawa.

Hii ina maana sio kweli wazawa wanabaniwa na kusababisha wasiitwe na kuisaidia Taifa Stars, kwani tunaona wazawa waliopo Simba, Yanga, Azam na Singida zenye idadi kubwa ya wageni ndio wanaoendelea kutawala timu ya taifa wakichanganywa na wazawa wanaocheza nje ya nchi.

Utabisha nini, angalia ukuta mzima wa Yanga Bakar Mwamnyeto, Ibrahim Bacca na Dickson Jon na mabeki wa pembeni wa Simba, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ au wale wa Azam  Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo, Nathaniel Chilambo ndio wanaounda ukuta wa Stars sambamba na makipa.

Wanapata nafasi hiyo kwa vile wanachuana na kuwashinda wageni waliopo katika vikosi vya klabu zao, mbali na kuiba mbinu zinazowabeba kwa manufaa ya Taifa Stars.

Halafu kuna timu yenye wazawa watupu, lakini kwa vile hawapati changamoto kubwa na wanaishi kwa mazoea, wanaishia kusikilizia Stars hewani tu, lakini bado kuna watu wanawatetea wanabaniwa. Wanabaniwa na nani wakati wachezaji wenyewe katika klabu zao na hawana watu wa kuwapa presha.

Hata kwenye mbio za ubingwa, kwa misimu mingi imeshuhudiwa timu ni zile zile Simba, Yanga na Azam zikiwa zinachuana kuwania ubingwa, huku vita ya kushuka daraja zikihusisha klabu zenye wazawa wengi na ambazo nyota wao hawana presha ya kugombea namba na wageni. Kwa nini tuendelee kujidanganya?!

Ili kufanya tuwe na wachezaji tegemeo kwa taifa ni kuhakikisha inajengwa misingi mizuri ya kuzalisha na kuibua vipaji vipya vitakavyopikwa na kujengewa uwezo wa kushindana bila kubweteka kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla badala ya kuwabania wageni.

Bahati nzuri kanuni za soka kwa sasa zinabana klabu, ikizitaka kuwa na timu za vijana ambazo zitashindana pia katika ligi zao kuanzia zile za U17 hadi U20.

Hii itasaidia kutengeneza hazina ya kesho iliyokuzwa katika ushindani, kiasi hata wanapoletewa kina Chama na Mutale wajao wawe tayari kuwamudu, sambamba na kufungua milango ya kuwashawishi kwenda kucheza soka nje.

Watu waliopo karibu na wachezaji hao wakiwamo menejimenti, marafiki na hata ndugu kama sio viongozi wa klabu wanazozitumikia, wasaidie kuwatia hamasa wapende kutoka nje wakachezea soka la  kulipwa kama ilivyokuwa kwa waliowatia hasira kina Mbwana Samatta, Simon Msuva, Novatus Dismas, Himid Mao na wengine ambao wamekuwa msaada kwa Taifa Stars.

Tukiwawajenga wachezaji wetu tangu wakiwa wadogo moyo wa ushindani na wa kupambana, haitakuwa ngumu kuwamudu wageni na kuchuana nao kama inavyoshuhudiwa kwa sasa kwa baadhi ya wachezaji waliopo Simba, Yanga na Azam wanaokula sahani moja na wageni na huiwezi kusikia hizi kelele zilizopo sasa.

Hali ikiwa hivyo, na wachezaji wazawa wakashinda kutoka nje ya nchi, itasaidia kuinua soka na hasa kwa upande wa Stars na hizi kelele za idadi ya wageni ipunguzwe au iongezwe yenyewe itajiseti kwa kipimo sahihi na hata wageni watakaokuwa wanasajiliwa watakuwa ni wale wenye faida.

Vinginevyo ni bora klabu ziendelee kuwagombania kina Chama na uzee wao kuliko kuwa na wazawa wazembe na wavivu wanaozikwamisha timu kufanya maajabu kimataifa na kuishia kulalamika kuitibulia Stars, wakati idadi ya wageni haifikii hata nusu ya wazawa waliobweteka na kuridhika kwa mafanikio machache.

Related Posts