Dar es Salaam. Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mohammed Khamis Abdulla, ameliagiza Shirika la Posta Tanzania kushirikiana na AzamPesa kuweka mifumo isiyoruhusu matumizi ya fedha taslimu kwa wateja wote wanaofika Kariakoo kufanya manunuzi.
Amesema endapo wateja watatumia mifumo ya kieletroniki kufanya manunuzi na kuepuka fedha taslimu, Serikali itapata kodi stahiki na hakutakuwa na migomo kwa wafanyabiashara.
Abdulla ameyasema hayo leo Julai 17, 2024 katika hafla ya utiaji saini wa mkataba wa kibiashara kati ya Shirika la Posta Tanzania na AzamPesa inayotoa huduma za kifedha kwa njia ya simu.
“Kila siku tunapata tatizo pale Kariakoo naomba Shirika la Posta mkaangalie namna ya kutatua, mtu asiende na fedha taslimu kununua bidhaa, miamala yote ifanyike kwa njia ya kieletroniki ili Serikali ipate kodi yake halali,”amesema.
Abdulla amesema makubaliano baina ya mashirika hayo mawili ni juhudi za Serikali katika kuinua uchumi wa kidijitali nchini na ipo tayari kufanya mabadiliko ya sheria na sera kufanikisha uchumi usiohusisha matumizi ya fedha taslimu.
Migogoro ambayo imekuwa ikiibuka Kariakoo ni wafanyabiashara na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yakihusisha masuala ya kodi jambo ambalo limekuwa likichangia wafanyabiashara kufunga maduka yao wakiwasilisha malalamiko ya kikodi.
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Maryprisca Mahundi, amesema ubunifu baina ya mashirika hayo utakwenda kugusa maisha ya wananchi wa chini kupata huduma za kifedha katika maduka yote ya Shirika la Posta.
“Mfumo huu wa malipo kwa njia ya simu umeunganishwa na mfumo wa malipo serikalini hivyo mtu akifanya manunuzi Serikali inapata mapato moja kwa moja,”amesema Maryprisca.
Naye Posta Masta Mkuu, Maharage Chande amesema makubaliano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kulitaka shirika hilo kushirikiana na sekta binafsi kuwafikia wananchi na kuimarisha utendaji.
“Ushirikiano huu ni sehemu ya mkakati wa shirika kukuza mapato baada ya biashara ya barua na vifurushi kupungua kutokana na mabadiliko ya teknolojia,”amesema.
Mkurugenzi wa AzamPesa, Ibrahim Malando amesema kupitia kampeni ya Ilipo Tupo, sehemu yeyote ilipo ofisi ya Shirika la Posta huduma ya AzamPesa pia itakuwepo.
“Mawakala na wateja watajisajili na kupatiwa huduma za kifedha na malipo mbalimbali ya Serikali,”amesema Malando.