Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemruhusu wakili Boniface Mwabukusi kufungua shauri la marejeo ya uamuzi uliomwengua kwenye orodha ya wagombea urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Hata hivyo, imekataa ombi la kusimamisha mchakato wa uchaguzi huo ambao sasa utaendelea kama ulivyokuwa.
Uamuzi huo umetolewa leo, Julai 17, 2024 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Salma Maghimbi baada ya kupitia maombi ya Mwabukusi na hoja zilizotolewa na wajibu maombi ambao ni TLS.
Mwabukusi alifungua shauri hilo Julai 11, 2024 katika Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.
Wakili huyo alikuwa miongoni mwa wagombea sita waliopitishwa na Kamati ya Uchaguzi ya TLS kugombea nafasi hiyo Juni 24, 2024.
Wagombea wengine waliopitishwa kuwania urais katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Agosti 2, 2024 jijini Dodoma ni Ibrahim Bendera, Emmanuel Muga, Revocatus Kuuli, Paul Kaunda, na Sweetbert Nkuba.
Ikielezwa ni kwa sababu ya doa la kimaadili, Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi TLS ilimuengua Mwabukusi kwenye kinyang’anyiro hicho kitendo anachokipinga.
Mwabukusi aliiomba mahakama kutoa ruhusa ya kufanya marejeo akidai Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TLS imemuengua pasipo kumpa nafasi ya kusikilizwa.
Anadai kulikuwa na ukiukwaji wa haki za binadamu na haki ya asili kwa kutoa hukumu bila kumshirikisha.
Pia aliomba zuio la mchakato wa uchaguzi wa TLS ngazi ya urais.
Akitoa uamuzi Jaji Maghimbi amesema kusimamisha uchaguzi kwa nafasi ya urais mahakama imeona hakuna sababu ya msingi ya kufanya hivyo na kwamba, baada ya kupewa ruhusa ana siku 14 za kufungua shauri la marejeo.
“Mleta maombi alikuja kwa ajili ya kuleta maombi ya kupata ruhusa ya kusajili marejeo na kuzuia uchaguzi katika nafasi ya urais, hivyo mahakama imekuruhusu kufanya Judicial Review, kama jinsi ulivyoomba,” amesema Jaji.
Mawakili 29 wa kujitegemea walijitokeza mahakamani kumtetea Mwabukusi katika shauri hilo, wakiongozwa na Mpare Mpoki, akisaidiana na Jebra Kambole, John Malya anayemwakilisha Pater Kibatala, Dickson Matata, Edward Heche na Ferdinand Makore.
Upande wa wajibu maombi ambao ni TLS wanawakilishwa na Wakili Steven Mwakiborwa na Hekima Mwasipu.
Awali, shauri hilo lilipoitwa mahakamani, Mpoki aliieleza Mahakama lilipangwa kutajwa na upande wa wajibu maombi wamekubali kuwa wamepokea nyaraka. Alisema mawakili wa kujitegemea wapatao 29 wakiongozwa na yeye watamtetea Mwabukusi.
Jaji Maghimbi baada ya kusikiliza hoja hizo, aliahirisha kwa muda shauri hilo hadi mchana wa leo Julai 17, 2024 alipotoa uamuzi.
Kesi ilipangwa kusikilizwa saa tatu asubuhi lakini iliahirishwa hadi saa 6.20 mchana. Jaji Maghimbi alisikiliza hoja za pande zote na kisha kuahirisha kwa muda kwa ajili ya kwenda kuandika uamuzi ambao aliutoa saa 9.04 mchana.