Ukatili watoto washtua wazazi, wavamia shule

Dar es Salaam. Baada ya kusambaa taarifa mitandaoni za mtoto Malick Hashim (6), mkazi wa Goba-Kinzudi kujeruhiwa na kitu chenye ncha kali shingoni na madai ya kuonekana sare za shule za mtoto zikiwa na damu, taharuki imeibuka kwa wakazi wa Mbande, baadhi ya wazazi wamevamia shuleni kuchukua watoto wao.

Taharuki kwa wakazi wa Mbande, wilayani Temeke imechangiwa na taarifa kwamba kuna nguo za mwanafunzi zenye damu zimeonekana eneo hilo.

Kwa mujibu wa wananchi waliozungumza na Mwananchi leo Julai 17, 2024 taarifa walizipata kutoka kwa baadhi ya wazazi kwamba nguo hizo zimeonekana jirani ya Shule ya Msingi Mbande.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema hapakuwa na tukio hilo, bali ni taharuki waliyopata wananchi baada ya kusambaa tukio la Goba- Kinzudi.

Amesema sababu nyingine ni kutokana na matukio ya kikatili kwa watoto yaliyokuwa yanajitokeza maeneo ya Mbagala Kuu na Toangoma.

“Kuna matukio ya ubakaji ambayo tunaendelea kuyafuatilia na unakuta kule Mbagala kumehamasika sana masuala ya ulinzi wa watoto, lakini wanawake kuhusu masuala ya kikatili yanayojitokeza,” amesema.

Kamanda Muliro amesema kutokana na hali hiyo, wananchi wakipata taarifa yoyote huwa wanapatwa na taharuki haraka kama iliyokuwa kipindi cha Panya Road (vijana waliokuwa wakifanya uhalifu mitaani).

“Nilipata taarifa hizo, lakini nimeongea na Kamanda wa Temeke ameniambia ni taharuki iliyosababishwa na taarifa za uongo na uzushi kwa hiyo watu wame –cool down (wametulia) na wenyewe hawajielewi baada ya kulidaka juujuu,” amesema Kamanda Muliro.

Mmoja wa walimu shuleni hapo aliyeomba asitajwe jina amesema hakuna tukio la mwanafunzi kufariki dunia shuleni hapo.

Amesema wameshangaa wazazi walifika huku wakiwa wamehamaki na kutaka kuchukua watoto wao.

“Tukio hilo halijatokea hapa shuleni, tumeshangaa wazazi wamekuja hapa kutaka kuchukua watoto wao baada ya kusikia taarifa hizo,” amesema.

Rose Madalali, miongoni mwa wazazi waliokwenda shuleni hapo amesema alikwenda kumfuata mwanaye, lakini baada ya kufuatilia alibaini hakuna ukweli wa tukio hilo.

Amesema amesikia jambo hilo kutoka kwa wazazi wenzake kuwa shuleni hapo kuna mwanafunzi amechinjwa, wakieleza walipata taarifa hizo kupitia mitandao ya kijamii.

“Baada ya kufika shuleni nimekutana na wazazi wengi kila mmoja akitaka kumchukua mtoto wake, lakini walimu walikuwa wanakataa kutokea tukio hilo na kugoma kufungua geti la shule,” amesema.

Rose amesema walimu baada ya kuona wazazi wanazidi kuongezeka, walifungua geti na kuruhusu wanafunzi kwa kuwatoa darasa moja hadi yote yakaisha.

“Kila mzazi akaondoka na mtoto wake kurudi nyumbani, lakini hakuna ukweli wowote,” amesema.

Kamanda Muliro amesema Malick (6) amejeruhiwa na kitu chenye ncha kali shingoni na msichana wa kazi anayejulikana kwa jina la Clemensia Cosmas ambaye anatafutwa na ni lazima apatikane.

“Jeshi la Polisi linamsaka Clemensia Cosmas kwa tuhuma za kumjeruhi kwa kitu chenye ncha kali maeneo ya shingoni mtoto Malick Hashim. Tukio hilo limetokea Julai 15, 2024 saa 12.00 jioni eneo la Goba Kinzudi, Wilaya ya Kinondoni,” amesema.

Amesema mtoto huyo alipelekwa Hospitali ya Mloganzila na baadaye amehamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili anapoendelea kupatiwa matibabu.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Aminiel Aligaesha amesema mtoto huyo alipokewa Jumatatu Julai 15, usiku na sasa anaendelea na matibabu.

“Kwa sasa suala hili lipo chini ya uchunguzi wa Jeshi la Polisi, hivyo sisi tunaendelea na matibabu wakati vyombo vya dola vikifanya kazi yake pindi watakapokuwa tayari watatoa taarifa,” amesema Aligaesha.

Kwa mujibu wa majirani, siku ya tukio walisikika watoto wakisema ‘Malick amejitaka shingoni’ kabla ya wao kwenda eneo hilo kutoa msaada.

Jirani aliyejitambulisha kwa jina moja la Janeth, amesema walishuhudia mtoto huyo akiwa amelala chini njiani karibu na nyumba yao.

Amesema awali walidhani tatizo hilo kalipata nje alipoanguka, hivyo walimtafuta dada wa kazi ambaye hakuonekana, lakini waliona michirizi ya damu kutoka ndani mpaka mtoto alipoangukia.

“Tunahisi wakati wa kitendo hicho kulikuwa na purukushani au alishatekeleza tendo hilo akahisi ameua akakimbia, mtoto akaweza kutoka ndani akaishiwa nguvu akaanguka,” amedai.

Jirani mwingine amesema kwa kipindi kirefu wamemuona msichana huyo wa kazi akiishi vizuri na waajiri wake.

Baba wa mtoto huyo, Hashim Kitumbi amesema wakati huu ambao mwanaye anaendelea kupigania uhai wake, analiomba Jeshi la Polisi liendelee kumtafuta binti anayedaiwa kufanya tukio hilo.

Hashim amesema mtoto wake alifanyiwa upasuaji Jumatatu usiku na anaendelea na matibabu mengine na kwa sasa wanaomba wadau walioguswa na tukio hilo kusaidia matibabu.

Amesema binti huyo wa kazi za ndani walimpata kupitia rafiki yao.

“Huyu kijana ni rafiki yetu na alituhakikishia ni mdogo wake, kwa uaminifu wake tukaona atakuwa sahihi kwetu. Hatukuwahi kuwasiliana na alikotoka zaidi tuliwasiliana na huyu kijana na haijawahi kutokea changamoto yoyote tumeishi na huyu binti kwa miezi sita,” amesema.

Amesema siku ya tukio baada ya majirani kumuona mtoto walimpigia mkewe simu na kumpa taarifa, alipofika nyumbani aliona tukio hilo na haraka alimchukua mtoto kumuwahisha hospitali.

Hashim amesema kijana aliyewapelekea binti huyo hajaonyesha ushirikiano tangu siku ya kwanza ya tukio, hivyo suala hilo wameliachia Jeshi la Polisi.

Kamanda Muliro amewataka wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine kuwa makini na wasaidizi wa kazi za ndani.

Amesema ni muhimu wahakikishe wanapata taarifa zao zote kabla hawajawaajiri na kuwaachia watoto na nyumba.

“Unapoletewa msichana wa kazi hujui ametoka wapi, unaweza kuletewa kichaa unamkabidhi mtoto. Nimetoa wito unapoletewa msaidizi wa kazi ni vizuri kujua aliyemleta ni nani, alikotoka, wazazi wake usiishie kuletewa na watu wa katikati. Tunaondoka tunawaachia nyumba na watoto wanaweza kuleta wezi pia ndani akishakusoma tu mazingira yako,” amesema Kamanda Muliro.

Mwanasaikolojia anasemaje?

Mwanasaikolojia ya afya na mtafiti, Dk Lusajo Kajula amesema kabla ya kuajiri msaidizi wa kazi za ndani ni muhimu kumchunguza hasa afya ya akili, ikiwezekana kumuuliza kama amewahi kupata ugonjwa wa akili au kama kwao kuna mgonjwa wa akili na ni muhimu kufahamu jamii anayotoka.

“Pia muhimu tuwasome watoto kwa kuwauliza kirafiki anamwonaje dada ni mzuri kwake? Amewahi kufanya vitendo vyovyote vibaya? Kabla ya kufanya kitendo kibaya kuna viashiria huonekana tuwasogeze karibu watoto na tusipuuze yale wanayotueleza,” amesema.

Dk Lusajo amesema mtu anaweza kufanya matukio ya ukatili kutokana na kupitia ukatili na kwamba, aliyepitia ukatili ni rahisi naye pia kufanya kwa mtu mwingine, hivyo ni muhimu kujua chimbuko lake na afya yake ya akili.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.

Related Posts