Yanga kuwafuata Wajerumani Sauzi kesho

KIKOSI cha Yanga kinatarajiwa kuondoka nchini kesho Alhamisi kwenda kuweka kambi ya wiki kama mbili katika jiji la Mpumalanga, Afrika Kusini.

Kama ambavyo awali Mwanaspoti iliporipoti, Yanga kupitia Msemaji wake Ally Kamwe amethibitisha safari hiyo ambapo kikosi hicho kitaondoka kesho saa 7 mchana.

Kamwe amesema, Yanga ikiwa huko itaweka kambi fupi pamoja na kucheza mechi mbili za mashindano ambayo wamealikwa.

“Klabu yetu imekuwa na tumepokea mialiko mbalimbali kutoka Asia, Ulaya na hapa Afrika, lakini uongozi kutokana na ratiba na mahitaji ya benchi la ufundi ukakubaliana na kwenda Afrika Kusini,” amesema Kamwe na kuongeza;

“Kule Afrika Kusini tumealikwa na wenyeji wetu, TS Galaxy ambao wameandaa mashindano maalum na tutaanza kucheza na Ausburg ya Ujerumani Julai 20.”

Kamwe amesema, baada ya mchezo huo Yanga itacheza mechi ya pili dhidi ya Galaxy yenyewe ambapo baada ya mechi hiyo wataenda Johannesburg ambalo watakuwa na ratiba ya jambo la kijamii.

“Tutakapomaliza ratiba ya jambo la kijamii tutakwenda Free State ambalo ndiko tutakapocheza mechi ya tatu dhidi ya Kaizer Chiefs katika mashindano maalum yaliyoandaliwa na kampuni ya Toyota.

“Tukimaliza mechi hiyo timu itarejea nchini Julai 30 kwa maandalizi ya mwisho ya kujiandaa na msimu wa Ligi na michuano ya Caf.”

Yanga itafanya Tamasha la Wiki ya Mwananchi, Agosti 4 kabla ya kucheza mechi za Ngao ya Jamii zitakazopigwa kati ya Agosti 8-11.

Yanga itakwaruzana na Simba Agosti 8, huku Coastal Union na Azam zitacheza mechi nyingine na washindi wataenda kukutana fainali .

Msimu uliopita Simba ilitwaa Ngao kwa kuifunga Yanga kwa penalti 3-1 baada ya dakika 90 kumalizika bila kufungana mechi zikipigwa Mkwakwani, jijini Tanga.

Related Posts