WATAWA WATATU WALIOFARIKI KWA AJALI WAZIKWA NDANDA,RAIS WA TEC ALIA NA MASHIMO KWENYE BARABARA ZA KUSINI.

Elizaberth Msagula,Lindi

Miili ya Watawa watatu wa Shirika la Mtakatifu Benedikto Abasia ya Ndanda Jimbo Katoliki la Mtwara, waliofariki dunia kwa ajali ya gari ijumaa Julai 12, 2024, imezikwa leo Julai 17,2024 katika makaburi ya Watawa huko Abasia Ndanda huku Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Tec Mhashamu Wolfgang Pisa akipaza sauti juu ya ubovu wa barabara katika Mikoa ya kusini.

Watawa hao ambao ni mapadri wawili,Padre.Cornellius Mdoe OSB,Padre Pius Boa OSB,na Bruda Bakanja Mkenda OSB,ajali ilikatisha uhai wao katika eneo la Mtualonga, barabara ya Masasi- Mnazi mmoja katika Halmsahauri ya Mtama mkoani Lindi wakitokea Ndanda ambako Julai 11,2024 kulifanyika sherehe za nadhiri za muda na za daima.

Akizungumza baada ya Misa Takatifu ya kuwaombea kabla ya maziko,Askofu wa jimbo Katoliki Lindi na Rais wa Baraza la Maaskofu TEC Mhashamu Wolfgang Pisa ameiomba Serikali licha ya jitihada kubwa inayofanya kurejesha miundombinu ya barabara iliyoharibiwa na mvua pamoja na Kimbunga Hidaya ingalia kwa jicho la huruma Barabara ya Masasi – Mnazi mmoja ambayo ina mashimo mengi, ili kuepusha ajali zinazotokea mara kwa mara na kugharimu maisha ya watu.

Akinukuu taarifa ya kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi juu ya chanzo cha ajali kuwa dereva alishindwa kulimudu gari baada ya kukwepa shimo lililopo barabarani na baadae kuingia kwenye korongo,Askofu Pisa amesema shimo hilo halikutakiwa kuwepo barabarani na kwakua bado shimo lipo panapaswa kuwekwa alama ili kuepusha ajali zisiendelee kutokea katika eneo hilo.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala amesema tayari barabara hiyo ya Kutoka Mtwara kupitia Mingoyo Mkoani Lindi mpaka Masasi tayari ipo kwenye mpango wa kutengenezwa upya,fedha zimeshapatikana na wakati wowote kazi itaanza.

Maziko hayo yalitanguliwa na Misa Takatifu ya kuwaombea marehemu hao iliyoaongozwa na Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Songea Damian Dallu na  kuhudhuriwa na Maaskofu wengine akiwemo  Mgashamu Wolfgang Pisa Askofu wa. jimbo Katoliki Lindi na Rais wa Tec,Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Mbeya Gervas Nyaisonga, Stephano Musomba Aksofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar Es Salaam  pamoja na Maabate 3.

Related Posts