Mwanza. Wafanyabiashara wadogo katika Soko la Magomeni lililopo eneo la Kirumba, Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, wameulalamikia uongozi wa manispaa hiyo kwa kuondoa meza zao walizokuwa wakitumia kufanyia biashara bila kuwapa taarifa yoyote.
Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatano Julai 17, 2024, baada ya uongozi wa manispaa hiyo kufika sokoni hapo na kuanza kuziondoa baadhi ya meza ambazo hazitumiki.
Hata hivyo, inaelezwa lengo la hatua hiyo ni kutaka kutoa nafasi kwa baadhi ya wafanyabiashara wadogo wanaofanya biashara zao kando mwa barabara kwa kuzitandika chini bidhaa zao.
Lakini baadhi ya wafanyabiashara sokoni hapo wanadai meza zinazoondolewa tayari zina wamiliki wake na baadhi hawajafungua biashara kutokana na dharura walizonazo.
“Walipaswa kuuliza kwanza kabla ya kuvamia tu na kuanza kuziondoa na kuzivunja,” amesema Anitha Paulini anayefanya biashara sokoni hapo.
Amesema miongoni mwa meza zilizovunjwa ni ya mama yake mzazi ambaye anauguliwa na alishatoa taarifa kwa uongozi wa soko.
“Hii meza ni ya mama yangu mzazi anamuuguza mdogo wangu toka mwaka jana, hata viongozi wa soko wanajua na wafanyabiashara wengine hapa wanajua, lakini meza yake imebomolewa nimejitahidi kuwaeleza lakini nimeambiwa niiondoe, sasa akija atafanyia wapi biashara? Haki ya sisi wafanyabiashara iko wapi?,” amehoji Paulini.
Akiunga mkono hoja hiyo, Datius Selestini, mbali na kuhoji utaratibu uliotumika kuvunja meza hizo, amedai hawakuwa na taarifa.
“Kwa kweli hawa watu wamenishangaza, sijui nani kawatuma au ni mamlaka waliyonayo wanatumia vibaya. Wala hatukuwa na taarifa yoyote, hata viongozi wa soko tulipowauliza nao wanasema hawana taarifa, tunaomba viongozi wa Serikali waingilie kati,” amesema Selestini.
Lakini akizungumzia sakata hilo, Mwenyekiti wa soko la Magomeni, Ramadhan Maganga amesema barua ya uondoaji wa meza hizo ameipokea leo asubuhi.
Amesema barua hiyo inasema kazi ya kuondoa meza zisizotumika sokoni hapo linafanyika kwa lengo la kutoa nafasi kwa wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao kando mwa barabara.
Akilizungumzia suala hilo, Ofisa Biashara ambaye pia ni Kaimu Ofisa Masoko Manispaa ya Ilemela, Yohannes Daud amesema kazi hiyo inafanyika baada ya uchunguzi kubaini baadhi ya watu wamejimilikisha meza zaidi ya moja na baadhi yao wanazikodisha na nyingine wamezitelekeza.
“Maeneo yote ya soko ni mali ya Halmashauri na mwenye mamlaka ya kukodisha ni mkurugenzi pekee. Lakini katika eneo hilo hamna mtu anayetozwa kwa kutumia eneo. Walipewa watu wafanyie biashara sasa kuna watu wanazikodisha hizo meza, wengine wamezitelekeza na wengine wanatumia maeneo hayo kama majalala. Ukienda kugusa unaambiwa yanamilikiwa na kikundi lakini wakati huohuo kuna ambao wanateseka barabarani, kitu ambacho sio utaratibu,” amesema Daud.
Amesema wameamua kufanya hivyo ili kuyatambua maeneo ambayo yametelekezwa ili yabaki wazi na kutoa nafasi kwa wengine.
“Kwa siku ya leo siwezi kusema ni meza ngapi zimeondolewa kwa sababu wanaendelea na kazi hiyo,” amesema Daud.