Dar es Salaam. Taasisi ya Utulivu Space imejipanga kueneza ujumbe wa amani na umoja miongoni mwa Watanzania kupitia matembezi maalumu yatakayofanyika Jumamosi Julai 20, 2024.
Katibu wa taasisi hiyo, Dk Mboni Dk Kibelloh amesema jana Jumanne Julai 16, 2024 kuwa lengo la matembezi hayo ni njia ya kurithisha vijana wa rika mbalimbali kufahamu chanzo cha utulivu wa Tanzania.
Amesema matembezi hayo yaliyoitwa ‘Matembezi ya Utulivu’ yatahitimishwa kwenye Viwanja vya Farasi, Masaki jijini Dar es Salaam ambako kutakuwa na burudani mbalimbali kwa vijana, akiwamo msanii wa Bongofleva, Sholo Mwamba.
Dk Kibelloh amesema matembezi hayo ni mwanzo, kwani yatahitimishwa kwa kufanyika tamasha kubwa la muziki baadaye Septemba 14, 2024.
“Matembezi hayo ya Jumamosi yataanzia Viwanja vya Farasi na yatakwenda hadi Daraja la Tanzanite, Hospitali ya Aga Khan na kurudi Daraja la Tanzanite na kuhitimishwa Viwanja vya Farasi.
“Tumetumia jina la Utulivu kwa kudumisha amani na utulivu uliopo miongoni mwa Watanzania ulioasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na zaidi ni kupitia lugha ya Kiswahili,” amesema.
Amesema vijana wengi wamezaliwa na kuikuta amani, hivyo wanataka kuwaambia vijana umuhimu wa kudumisha amani na umoja pamoja na chanzo cha amani ya Watanzania.
Kuhusu uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika baadaye mwaka huu, Dk Dk Kibelloh amewataka vijana kuchagua viongozi vijana na kutumia demokrasia ya kupiga kura kwa amani na utulivu.
Kwa upande wake, Ofisa Sanaa Mwandamizi kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Abel Ndaga amesema baraza hilo itasimama na Taasisi ya Utulivu Space kwa lengo la kuhakikisha amani na utulivu unadumishwa.