Watoa huduma za afya watakiwa kuzingatia vipaumbele vya Serikali

Dar es Salaam. Watoa huduma za afya wametakiwa wafuate vipaumbele vya Serikali katika utoaji wa huduma ili kuleta matokeo chanya.

Mkurugenzi wa Huduma za Afya wa Wizara ya Afya, Dk Ahmad Makuwani amesema hayo Jumatatu Julai 15, 2024 wakati wa ufunguzi wa kongamano la huduma za afya (Health Care Excellence Symposium) lilioandaliwa na Shirika la AHEAD inc jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya shirika hilo katika utoaji wa huduma za afya, elimu na kilimo.

Dk Makuwani amesema ikiwa watoa huduma watazingatia vipaumbele vya Serikali, itasaidia kukabiliana na changamoto za afya nchini.

Amewataka watoa huduma kutozingatia vipaumbele vyao binafsi badala yake wafuate miongozo ya Serikali ikiwamo kuwepo kwa vifaatiba vya kutosha na majengo imara ili kukabiliana na changamoto mbalimbali.

“Serikali inapongeza na kutambua mafanikio ya AHEAD kupitia miradi yake hususani katika sekta ya afya na hata uamuzi wa kuandaa kongamano hili muhimu katika kutathimini hali ya utoaji huduma katika sekta ya afya,” amesema.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa AHEAD, Dk Donna Williams-Ngirwa amesema imekuwa safari ya kustaajabisha kwao tangu walivyohamia Tanzania kutoka nchini Marekani Julai 1974.

Amesema  baadaye wazazi wao walianzisha Shirika la Ujasiri katika Afya, Elimu na Maendeleo ya Kilimo.

“Sisi kama watoto wa waanzilishi wa Shirika la AHEAD tunaendelea na kazi ambayo wazazi wetu waliianzisha kuhakikisha programu za kudumisha maisha zinafika hadi maeneo ya mbali yenye uhaba wa rasilimali na zinakuwa endelevu.

“Katika kuadhimisha miaka 50 ya mafanikio ya kihistoria, tunaona fahari kuwa mwenyeji wa kongamano hili la ubora wa afya lenye dhamira ya kuendeleza afya kwa njia ya uongozi, diplomasia, uvumbuzi na ushirikiano,” amesema Dk Williams-Ngirwa.

“Kongamano linalenga kuwa chachu ya mabadiliko katika sekta ya afya nchini Tanzania, likisisitiza umuhimu wa kutoa huduma bora za afya kwa watu wetu na kwa kutumia watu wetu,” amesema Dk Williams-Ngirwa..

“Tanzania ina watoa huduma bora wa afya. Tunahakikishaje wananchi wote wanapata huduma bora?”

Mada zilizojadiliwa  katika kongamano ni afya ya akili, mfumo wa afya ya kinywa, matibabu ya watoto na radiolojia, huku hotuba muhimu ikitolewa na Dk Winnie Mpanju-Shumbusho, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na mwanzilishi wa AHEAD Tanzania.

AHEAD imekuwa mfano wa kuigwa katika kukuza diplomasia ya watu na kupunguza vifo vya uzazi, kuongeza viwango vya chanjo na kusaidia katika miradi mingine inayotekelezwa vijijini katika wilaya za Meatu, Kishapu, Kisarawe na miradi yao ya sasa huko Maruku, Bukoba.

Related Posts