Mchungaji kortini akidaiwa kuua kwa kukusudia

Mwanza. Ernest George (37), amepandishwa kizimbani na kusomewa shitaka la mauaji ya kukusudia ya dereva, Majuto Seif.

George, ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la Tanzania Assembly of God (T.A.G), maarufu Mchungaji George amesomewa shitaka katika kesi ya mauaji namba 19830/2024, leo Jumatano Julai 17, 2024 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza.

Amesomewa shitaka hilo na Wakili wa Serikali, Evance Kaiser mbele ya hakimu, Stella Kiama.

Kaiser amedai mshtakiwa na wenzake wanne ambao hawakuwapo mahakamani walitekeleza mauaji ya dereva huyo Juni 27, 2024 katika eneo la Lugeye wilayani Ilemela, mkoani Mwanza.

Anadaiwa kutenda kosa hilo kinyume cha vifungu vya 196 na 197 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu namba 16 na marejeo ya mwaka 2012.

Baada ya kusomewa shitaka hilo, hakimu Stella amesema Mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria ya kusikiliza shauri hilo, hivyo amemtaka mshtakiwa kutojibu chochote.

“Shitaka linalomkabili mshtakiwa Mahakama hii haina mamlaka ya kutoa maelekezo yoyote, kwa hiyo zaidi ufahamu shitaka hili halina dhamana, hivyo Mahakama itapanga tarehe kwa ajili ya kushughulikia upelelezi na utakapokamilika shauri liende katika Mahakama iliyo na mamlaka ya kulisikiliza,” amesema hakimu.

Baada ya kauli hiyo, hakimu ameahirisha shauri hilo hadi Julai 31, mwaka huu saa 4.30 asubuhi litakapoitwa kwa ajili ya kutajwa. Mshtakiwa amepelekwa rumande.

Related Posts