Dar es Salaam. Ili kuondoa changamoto na upungufu uliopo katika uendeshaji wa mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT), Serikali imeshauriwa kuongeza usimamizi, kuzingatia rasilimali watu yenye utaalamu na kuanzisha bodi itakayoshughulikia masuala ya usafiri nchini.
Ushauri huo umetolewa leo Julai 17, 2024 wakati wa mjadala ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kupitia Mwananchi X Space ukiwa na mada isemayo ‘Mkopo wa mabasi 100 ya mwendokasi, utasaidia kupunguza changamoto za mradi huo, nini kifanyike?’
Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Oscar Mkude amesema wakati mradi wa mabasi yaendayo haraka unaanzishwa wengi walikuwa na matarajio makubwa ya kurahisisha safari zao.
“Dar es Salaam ni Jiji linalokua kwa haraka kwa maana ya idadi kubwa ya watu wanaoingia, usafiri ni muhimu kwenda katika shughuli zao za kila siku za kiuchumi katika ujenzi wa nchi,” amesema.
Mkude amesema kadri muda unavyoenda mradi hauakisi kile kilichokuwa kinatarajiwa ulipoanzishwa.
“Hata ukiwasikiliza viongozi wanakosa ushahidi wa kutosha kuthibitisha kile kilichosemwa mwanzo,” amesema.
“Ndani ya muda mfupi wamebadilishwa viongozi wengi na kuacha maswali mengi, kwa nini wanaondoka haraka. Wengine wanavyoondoka kumekuwa na maneno na wengine kuonywa hali inayoonesha kuna shida katika usimamizi,” amesema.
Mkude amesema awali mradi huo ulipobuniwa kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia (WB) lengo lilikuwa utekelezwe kwa mfumo wa sekta binafsi kwa kushirikisha taasisi za kimataifa zenye uzoefu mkubwa.
“Tatizo la msingi si vifaa vya kufanyia kazi lakini kilichotufikisha hapa ni kushindwa kusimamia biashara hii. Sasa kuleta vifaa vingine unakuwa hujawatatulia mkwamo wa kushindwa kuendesha biashara,” amesema.
Mkude amesema mashirika ya umma yana matatizo yanayoyafanya yashindwe kujiendesha kwa faida, ikiwemo kuwa na ufanisi mdogo hata kwa kuwa na watendaji wasiokuwa na uwezo wakuleta tija.
“Miradi mingi ina sura ya kisiasa na maamuzi yake yanaingiliwa, malengo yake na matamanio mengine ambayo ni ya kisiasa zaidi, sasa hiyo haiondolewi kwa kuleta mabasi mengine mapya,” amesema.
Amesema miradi hiyo baadhi ya watendaji wanafanya ufisadi na wanaichukulia kama sehemu ya kujibinafsisha.
“Suluhisho ni kuwatoa hao ili apatikane mwekezaji mwingine ambaye ataweza kuendesha,” amesema.
Awali akichokoza mada hiyo, Mhariri wa Uchumi gazeti la Mwananchi, Ephraim Bahemu amesema changamoto iliyopo kwenye mradi wa BRT ni zaidi ya upungufu wa mabasi.
Amesema wakati mradi huo unaanza miaka saba iliyopita ulikuwa ukitoa urahisi kwa abiria kwani hata mgeni angeweza kufika aendako kwa urahisi tofauti na sasa.
Amesema iwapo mradi ungetekelezwa kama ulivyopangwa ungebadilisha hali ya usafiri wa umma katika Jiji la Dar es Salaam kwa kuleta uzoefu mpya.
“Changamoto ya mradi wa mabasi yaendayo haraka ni zaidi ya mabasi, mifumo ya kidijitali iliyokuwapo mwanzo ilirahisisha huduma lakini sasa ni tofauti kuanzia malipo ya tiketi na hata huduma ndani ya vituo na mabasi yenyewe.
Amesema awali abiria alikuwa anaweza kutunza nauli kupitia kadi ya BRT na hakukuwa na usumbufu wa kupanga foleni ya kulipia tiketi kama ilivyo sasa. “Mifumo ya kuskani kadi na tiketi ilikuwa inafanya kazi”
Bahemu amesema ile neema, furaha na urahisi ambao watu walikuwa wakipata kwenye mradi huu imegeuka kuwa kero.
Amesema kwa sasa mabasi yanachelewa vituoni na kuna wizi ndani ya mabasi sababu ya kubanana.
“Ladha ya usafiri huo ambao ulikuwa na viwango vya kimataifa imepotea na sasa usafiri huo umekuwa kama daladala na wakati mwingine afadhali ya daladala,” amesema.
Mtaalamu wa masuala ya usafirishaji, Edward Munanu amesema mradi wa mabasi yaendayo haraka hauendeshwi kitaalamu.
Amesema licha ya kuwapo wataalamu wa usafirishaji nchini, hawatumiki kukiwa na dhana kwamba kila mtu anaweza kuendesha magari pasipo kuangalia taratibu zake.
“Kuanzishwe bodi ya usafiri, kama ambavyo zipo bodi za wanunuzi, uhasibu. Tunakuwa na imani kwamba mtu akiwa na magari 100 ndiyo mtaalamu mwenyewe hapana, ukiangalia kwenye uhasibu wanazungumza vizuri kampuni ikifa wanaangalia ni nani alikuwa na jukumu la kuangalia fedha,” amesema.
Munanu amesema kwenye sekta ya usafiri kuna tatizo kila mtu kuonekana anaweza kufanya kazi hiyo, hivyo hakuna utaalamu unaohitajika.
Amesema anaunga mkono hatua ya Serikali kuleta mabasi mapya lakini ni umuhimu wataalamu wa ndani watumike kuyasimamia kwa ufanisi zaidi na matatizo mengine yaangaliwe bila kufunikwa.
Mdau wa Usafirishaji, Honest Temu amesema uteuzi wa watu kusimamia miradi bila kuwa na utaalamu ni sababu inayochangia mradi wa mwendokasi kurudi nyuma.
Ameshauri kuwe na utaratibu wa kuwafanyia usaili wanaoajiriwa kusimamia miradi ya Serikali kabla ya kuajiriwa ili waeleze namna watakavyosaidia kukuza miradi hiyo.
“Tatizo kubwa ni usimamizi, nafasi ya kuteua watu kusimamia miradi bila kuwa na taalamu ndiyo inaturudisha nyuma, watu hawa wawe wanafanyiwa usaili na waeleze baada ya kupewa mabasi 300 wataleta faida kiasi gani,” ameeleza Temu
Amesema uendeshaji wa mradi wa mwendokasi, changamoto kubwa ni ununuzi wa vipuri ambayo inaweza kutatuliwa kwa Serikali kufanya mazungumzo na wauzaji wa vipuri hivyo na kuwaelekeza kuja kutoa huduma hiyo nchini.
“Serikali ilipaswa kabla ya kuanzisha mradi huu ingefanya tathmini ya hasara ni kiasi gani, upatikanaji wa vipuri utakuwaje, kwa sababu ukiangalia gharama kubwa zipo kwenye uendeshaji wa mradi,” amesema.
Mdau wa usafiri na Katibu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma-Bara), Eugene Kabendera amesema mkopo wa mabasi 100 ya mwendokasi hauwezi kupunguza changamoto isipokuwa unaenda kuwabebesha mzigo Watanzania.
“Hata yakiongezeka mabasi 1,000 kwa utaratibu tunaouona hapa tulipofikia hauwezi kupunguza changamoto. Huwezi kuziba shimo la panya kwa kutumia mkate, panya wataendelea kula na huwezi kuhifadhi barafu kwenye jua,” amesema.
Kabendera amesema Julai 15, 2024 Msajili wa Hazina alikiri mfumo wa kukusanya fedha una mianya mingi na watu wanajinufaisha.
“Mkopo huu wa mabasi 100 unaenda kubebesha mizigo Watanzania ambao ni walipa kodi lakini matokeo yake hauwezi kwenda kupunguza changamoto,” amesema.
Amesema lazima kama nchi kujisahihisha na kujitathimini kwa kujiuliza kuna shida gani, kiasi kwamba kila miradi inayoanzishwa na Serikali inafika mahali inakufa.
“Kuna miradi mingi inakufa kwa mambo hayahaya, usikute hata mradi wa reli ya kisasa (SGR) utakuja kufa kwa matatizo haya, hata matengenezo hayafanyiki,” amesema.
Kabendera amesema inasikitisha kila kiongozi anayetoka anasikitika na kukosoa, akieleza alitarajia viongozi watajisahihisha lakini mambo yamekuwa yaleyale.
“Sasa hivi mtu huna hamu ya kupanda tena mwendokasi, bora uchukue usafiri mtandao au kupanda bajaji kama watu wa Kimara, daladala zimekuwa nyingi kwa sababu mwendokasi imeshindwa kutatua mahitaji ya usafiri,” amesema.
Kwa upande wake, Adam Mpambe akichangia mada amesema mkopo wa mabasi hayo utasaidia kupunguza changamoto za mradi huo.
“Ukiangalia Serikali imeendeleza mradi wa mabasi yaendayo haraka upande wa Mbagala, hivyo kuna uhitaji wa kuongeza mabasi ili wananchi wapate huduma ya usafiri. Serikali imefanya jambo jema kukopa kwa ajili ya mabasi ili kutatua changamoto ya usafiri,” amesema.
“Changamoto kwa upande wa Serikali ni usimamizi wa mradi, unaweza kujiuliza kuna shida gani kwa hawa wanaosimamia miradi. Mabasi yanaharibika, unajiuliza hatuna vipuri? hatuna mafundi wazuri, mabasi yanaegeshwa bila sababu ya msingi,” amesema.
Amesema kama changamoto hizo haziwezi kutatuliwa itakuwa hasara kubwa, kwani Serikali itakuwa na deni na mabasi hayafanyi kazi.
Mkuu wa Idara ya Usafirishaji na Biashara katika Chuo cha Usafirishaji Tanzania (NIT), Dk Prosper Nyaki amesema mahitaji ya abiria ni zaidi ya 370,000 kwa siku kwa mujibu wa taarifa za Jiji la Dar es Salaam.
“Tunahitaji magari 300 hadi 370, lakini kwa sasa Udart wanaendesha mabasi 140 hadi 150 ukisema unaongeza mabasi 100 bado tatizo litaendelea kujitokeza,” amesema.
Amesema Serikali inatakiwa ijizatiti iwekeze kwa nguvu zaidi kwa kuhakikisha inaongeza uwezo wa magari ili kuchukua abiria kama walivyoweka kwa kuakisi matarajio wakati unaanzishwa.
“Kuendesha magari haya kunaendana na gharama, ukiangalia hapa Dar es Salaam asubuhi kuna abiria kwenda katikati ya mji, jioni kurudi nje ya mji wakati wa kwenda magari yanajaa na kurudi yanakuwa matupu,” amesema.
Amesema kutokana na hali hiyo gharama za uendeshaji zinaongezeka kwa hiyo Serikali inatakiwa iangalie namna ya kutoa ruzuku kwa magari ya usafiri wa umma na itavutia wawekezaji wapya kuwekeza.
“Vilevile Serikali iangalie namna ya kuhusisha taasisi zingine katika kupanga ramani ya huu mji kuwe na shughuli karibu na hii miradi kama nyumba, maduka na mabenki ili kuhakikisha muda wote mabasi yanajaza abiria,” amependekeza.
Amesema wataalamu ni changamoto kubwa ndani ya mradi huo, akieleza katika usafiri kuna wataalamu akiwataja mainjinia wanaoyajua magari kiundani na wanajua ni wakati gani wafanye matengenezo.
“Katika uendeshaji kuna shida hasa wanaosimamia, na madereva wanachangia kuharibu magari,” amesema.
Amesema mradi unahitaji wataalamu wa Tehama watakaosaidia katika ukusanyaji wa mapato tofauti na ilivyo sasa wanafanya kazi kwa mfumo wa kawaida.
“Wanakusanya mapato lakini hawana kumbukumbu za kutosha labda tungepata wataalamu wa eneo hilo ingesaidia kutoa tiketi mtandao, ambazo abiria anaweza akaitumia taratibu na kutoa taarifa sahihi kwa watumiaji,” amesema.
Dk Nyaki amependekeza iwepo bodi ya usimamizi ya usafirishaji kwa kuhakikisha vyombo vya usafiri vinaendeshwa na watu mahiri katika eneo hilo na wanajua kinachotakiwa kufanyika.
“Tuache kutumia siasa zaidi katika eneo hili la usafiri na tuache wataalamu wafanye kazi zao kwa kuzingatia taaluma. Pia udhibiti wa rushwa katika eneo la usimamizi na uagizwaji wa magari unahitajika,” amesema.