Baada ya CUF na Chadema hatimaye Kambaya na kundi lake waangukia CCM

Dar es Salaam. Mwanasiasa, Abdul Kambaya na wengine wanaodaiwa kuwa zaidi ya 800 wamejiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Sehemu ya kundi hilo ndiyo wale ambao Machi mwaka 2023 walitangaza kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutokea Chama cha Wananchi (CUF).

Kambaya na wenzake zaidi ya 600 Machi mwaka jana walitangaza kukihama chama cha CUF na kuhamia Chadema.

Licha ya mapokezi makubwa waliyoyapata kutoka Chadema, haikuchukua hata mwezi kwa Kambaya na wenzake kujiondoa katika chama hicho.

Uamuzi wa kuondoka Chadema waliutangaza Mei 6, 2024 na tangu hapo haikujulikana wanakwenda kuwa wanachama wa chama kipi.

Msingi wa uamuzi wa kujiondoa kwao ni kile kilichoelezwa na baadhi yao kuwa, kuna ukiukwaji wa makubaliano uliofanywa na Chadema baada ya kujiunga nacho.

Lakini, kabla ya hamahama zake katika vyama mbalimbali vya siasa, Kambaya amewahi kuwa Mkuu wa Kitengo cha Habari CUF.

Mwanasiasa huyo na wenzake ndani ya CUF ndiyo waliokuwa sehemu ya washiriki wa vuguvugu lilimuondoa Maalim Seif Sharif Hamad katika chama hicho na baadaye alijiunga na ACT Wazalendo.

Kambaya ametangaza kujiunga na CCM leo, Julai 17, 2024 katika mkutano wa hadhara wa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla uliofanyika katika Uwanja wa Mwinyijuma jijini Dar es Salaam.

Uamuzi wa Kambaya na wenzake kujiunga na CCM, amesema unatokana na uungwana na Rais Samia Suluhu Hassan akidai amewahi kusifiwa hata na viongozi wa vyama vya upinzani.

Amesema kama viongozi wakuu wa vyama vya upinzani wanasifu utendaji wa Rais Samia, wao ni nani waonekane wa ajabu kujiunga na CCM.

Kutokana na uamuzi wa Kambaya, Makalla amesema kwa kuwa aliwahi kuisumbua CCM katika eneo la Kinondoni kwa sasa atatumika kuisumbua CUF katika chaguzi zijazo.

Related Posts