Tuzo ya ushindi Sabasaba iwe nguzo kutoa huduma bora – Dk. Yonazi

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dk. Jim Yonazi amesema tuzo waliyoipata katika maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) iwe nguzo ya kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.

Ofisi ya Waziri Mkuu ilipata tuzo ya ushindi wa kwanza kwa kundi la watoa huduma bora na banda bora ngazi ya wizara zilizoshiriki katika maonesho hayo.

Ameyasema hayo Julai 17,2024 baada ya kupokea tuzo hiyo ofisini kwake jijini Dodoma ambapo ameshukuru viongozi wa ofisi hiyo na taasisi zake kwa maandalizi mazuri.

Amesema tuzo hiyo itawezesha ofisi kufikia malengo ya Serikali na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kuleta tija kwa Taifa.

“Naamini nwakani tunaweza kufanya vizuri zaidi kwa kuchukua ushindi wa jumla na si katika utoaji huduma bora na banda bora, hivyo hii iwe chachu ya kuamsha morali ya kazi kwa watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu,” amesema Dk. Yonazi.

Naibu Katibu Mkuu wa ofisi hiyo, Anderson Mutatembwa, amepongeza timu nzima iliyoshikiri katika maandalizi hayo na kusema ni dalili nzuri inayoonesha utekelezaji wa maagizo na miongozo inayotolewa na viongozi wa ngazi za juu.

Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Uwekezaji na Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Condrad Millinga, amesema kupitia maonesho hayo wananchi waliofika katika banda hilo walipata nafasi ya kufahamu majukumu yanayotekelezwa na ofisi hiyo pamoja na taasisi zake.

“Wanachi walipata elimu kuhusu tunavyotekeleza majukumu pamoja na kuwahudumia kwa ubora, hii ilichangia kuongeza tija ya uwepo wa banda la Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake katika maonesho hayo,” amesema Millinga.

Related Posts