Mbeya. Aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo Kuu la Magharibi (KMT-JKM), Dk Alinikisa Cheyo amepata mrithi wake baada ya Mchungaji Robert Pangani kuteuliwa kushika nafasi hiyo.
Mchungaji Pangani atasimikwa kukalia kiti hicho Juni 2 mwaka huu, huku Rais Samia Suluhu Hassan akitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo.
Mchungaji Pangani amechaguliwa na Mkutano Mkuu wa Jimbo uliofanyika Novemba 2, mwaka jana.
Akizungumzia sherehe hizo jana jioni Aprili 17, 2024, Askofu Kiongozi wa kanisa hilo, Kenani Panja amesema Askofu mteule Pangani atakuwa wa tatu kushika nafasi hiyo baada ya watangulizi wake a Askofu Yohana Wavenza na Askofu Alinikisa Cheyo walioongoza kanisa hilo katika vipindi tofauti.
Amesema mbali na kusimikwa kiongozi huyo kutakuwa na ibada kubwa ya kumuombea Rais Samia itakayofanyika Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji (Teku) Jijini Mbeya itakayohudhuriwa na viongozi wa Kanisa la Moravian duniani, wakiongozwa na Mtendaji Mkuu, Mchungaji Jorge Boytler.
“Tunatarajia kuwa na ugeni mkubwa kutoka mataifa mbalimbali nchini na viongozi wa Kanisa la Moravian, hivyo tutakuwa na ugeni mkubwa sana,” amesema.
Akizungumza kwanini wameamua kumualika Rais Samia, Askofu Panja amesema ni kutokana na mchango wake mkubwa anautoa kwa Taifa anapoliongoza huku amani na utulivu ukiwa umetamalaki.
Katibu Mkuu wa kanisa hilo ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya maandalizi, Israel Mwakilasa amesema wanatarajia kuwa na viongozi wa dini wa ndani na nje ya nchi kutoka mataifa sita duniani sambamba na umoja wa jumuiya ya maridhiano.
Ameyataja mataifa yatakayoshiriki sherehe hizo ni Uswisi, Ujeruman, Uingereza, Zambia, Malawi, Denmark na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Mwaisaka amesema kutakuwa na tuzo malumu kwa wadau mbalimbali wenye mchango mkubwa kwa kanisa itakayotolewa na Rais Samia.