Kansela wa zamani wa Ujerumani Angela Merkel amestaafu tangu karibu miaka miwili na nusu. Taasisi ya uchunguzi wa maoni ya YouGov ilifanya uchunguzi wakilishi kwa watu 2,300 nchini Ujerumani kutaka kufahamu namna wanavyomkumbuka.
Asilimia 61 walisema hali ya nchi imekuwa mbaya tangu Merkel aondoke madarakani. Walipoulizwa kuhusu sababu za hili, asilimia 28 walisema kuwa “uongozi mbovu” ya serikali ya sasa ya mrengo wa wastani wa kushoto ndio wa kulaumiwa.
Muungano wa vyama vya Social Democrats, SPD, watetezi wa mazingira, die Grüne, Waliberali Mamboleo, Free Democrats, FDP, walirithi serikali kuu ya mseto ya Merkel ya iliyoudwa na vyama vya Christian Democratic Union (CDU)/Christian Social Union (CSU) na SPD baada ya uchaguzi mkuu mwaka wa 2021. Ni robo tu ya wale waliohojiwa walisema kwamba hali ya maisha nchini Ujerumani imesalia kuwa sawa tangu wakati huo.
Msimamo wa kweli wa Merkel na uyanikifu
Haijulikani iwapo Angela Merkel anafahamu kuhusu utafiti huu, lakini pasina shaka anafahamu kuwa warithi wake walikuwa na bado wanapaswa kukabiliana na migogoro mibaya: Vita vya Urusi dhidi ya Ukraine, mfumuko wa bei uliotokana na vita hivyo, kupanda kwa bei ya nishati na vita vya Israel na Hamas katika Mashariki ya Kati.
Soma pia: Angela Merkel atajishughulisha na nini baada ya kustaafu?
Mbali na hayo, kuna mgawanyiko unaoongezeka kila mara wa kijamii, upopulisti wa mrengo mkali wa kulia kote Ulaya, ukiritimba unaokwamisha shughuli na miundombinu iliyoharibika nchini.
Merkel alikuwa myakinifu sana na asiye na hisia wakati wa miaka 16 alioiongoza serikali ya Ujerumani kuanzia 2005 hadi 2021. Tangu kuondoka kwake kwa hiari, Merkel kwa kiasi kikubwa amejiweka mbali kabisaa na macho ya umma – kama ambavyo alisema angefanya.
Alikuwa mkuu wa kwanza wa serikali ya Ujerumani ya baada ya vita vikuu vya pili vya dunia kuondoka madarakani kwa hiari yake mwenyewe alivyoamua kutogombea tena uchaguzi mwaka wa 2021. Na yeye ndiye wa kwanza ambaye anaonekana kutotaka kujimulika.
Hata hivyo, watu wengi wamemkumbuka na kumpongeza kwa kutimiza miaka 70 ya kuzaliwa – kama Rais wa Shirikisho Frank-Walter Steinmeier, ambaye alihudumu mara mbili katika serikali ya Merkel kama waziri wa mambo ya nje kupitia chama chake, SPD.
Katika salamu zake rasmi za siku ya kuzaliwa, Steinmeier alimsifu Merkel kama “mfano wa kuigwa na alama mahususi ya demokrasia yetu.”
Kitu cha kipekee kwake, alisema, ni kwamba maisha ya Merkel yanaweza kugawanywa karibu kwa usawa katika awamu mbili: “Miaka 35 ya kwanza hadi kuanguka kwa Ukuta wa Berlin. Na miaka 35 ya pili katika uhuru uliotafutwa kwa muda mrefu,” alisema mkuu huyo wa nchi.
Soma pia: Merkel ajibu maswali ya wabunge kwa mara ya mwisho
Aliendelea: “Wakati wote ilikuwa muhimu kwako kusisitiza thamani ya uhuru na jamii iliyoelimika. Hoja zako zilikuwa za kusadikisha kwa sababu ulijua vyema zaidi kutokana na uzoefu wako mwenyewe thamani isiyokadirika ya kuishi katika demokrasia ya kiliberali.”
Angela Merkel alianza siasa baada ya kuanguka kwa Ukuta
Merkel daima amekuwa akikabiliwa na asili yake katika iliyokuwa Ujerumani Mashariki ya ukomunisti, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani (GDR). Alikuwa mwanafizikia alieondolewa kwenye siasa, na kujikuta tena katika siasa wakati wa kipindi cha kusisimua cha mabadiliko baada ya Novemba 9, 1989, wakati Ukuta wa Berlin ulipoanguka, baadaye sana kuliko wanasiasa wengi wanaume wa Ujerumani Magharibi. Hili linadhihirika katika makala mpya ya filamu yenye sehemu tano inayorushwa na shirika la utangazaji la ARD yenye kichwa: “Miaka ya Hatima ya Kansela Mwanamke.”
Katika makala hiyo, Merkel mwenyewe anasimulia jinsi alivyohamia katika ghorofa ya nyumba chakavu Berlin Mashariki mwaka 1984, katika siku yake ya mwaka wa 30 wa kuzaliwa. Ndoa yake ya kwanza ilikuwa imevunjika. Baba yake, mchungaji, alikuja kumtembelea. “Alitazama huku na huko na badala ya kunipongeza, alisema: Bado haujafika mbali,” Merkel alisimulia miaka 40 baadaye.
Soma pia: Biden na Merkel wakutana mjini Washington
Haiwezi kusemwa hivyo katika miaka iliyofuata. Njia ya Merkel kutoka naibu msemaji wa habari wa waziri mkuu wa kwanza kuchaguliwa kwa uhuru wa GDR hadi waziri wa mazingira wa shirikisho la Ujerumani iliyoungana tena hadi enzi ndefu ya ukansela wake inaonekana kuwa ya ajabu, karibu na njozi. Kazi ambayo yumkini ingeweza tu kuanza kwa njia hii wakati wa miaka ya kuunganishwa tena kwa mataifa mawili ya Ujerumani.
Makosa ya miaka ya Merkel
Tangu kustaafu kwake, Merkel amejitokeza hadharani mara chache sana, wakati mwingine kwa njia ya kushangaza kabisa, kama Mei mwaka huu, kwenye tafrija ya kustaafu kwa Waziri wa zamani wa Mazingira, Jürgen Trittin wa Chama cha Kijani, mwanasiasa ambaye hakuwa karibu naye. Mkutano kati ya Merkel na Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama mjini Berlin mwezi Mei 2023 ulipamba alau vichwa vichache vya habari. Vinginevyo, tunasikia kwamba Merkel yuko bize kuandika kitabu chake, kinachotazamiwa kuchapishwa baadaye mwaka huu.
Merkel kwa kiasi kikubwa ametengwa na chama chake cha CDU, na hajahudhuria mkutano wowote wa chama tangu Desemba 2021. Katika siku yake ya kuzaliwa, naibu kiongozi wa kundi la wabunge wa chama hicho Jens Spahn alisifu urathi wa Merkel, lakini katika mahojiano na jarida la habari la Focus, pia alitaja yale aliyoeleza kuwa makosa matatu makubwa aliyoyafanya.
“Uhamiaji mkubwa usio halili tangu 2015 umedhoofisha na kulemea jamii ya Ujerumani,” alianza waziri huyo wa zamani wa Afya.
Kosa namba mbili? “Tulipaswa kushughulika na Urusi ya Putin kwa njia tofauti sana kuanzia mwaka 2014 [unyakuzi wa Urusi wa rasi ya Crimea].”
Kulingana na Spahn, kosa la tatu lilikuwa kuondoa nishati ya nyuklia baada ya maafa ya 2011 ya mjini Fukushima.
Ukiwauliza wawakilishi wa serikali ya sasa ya mseto, wengi watasema kuwa wakati wa Merkel serikalini ulikuwa na sifa ya kuendelea, kwa kuzingatia imani thabiti kwamba kungefanyika mabadiliko madogo iwezekanavyo kwa nchi. Hii, wanasema, ina maana kwamba mabadiliko sasa yanapaswa kufanywa kwa haraka: ukuzaji wa mifumo ya kidigitali, mabadiliko ya nishati, kukabiliana na uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi. Na katika ulimwengu unaokabiliwa na kitisho kinachoongezeka cha itikadi kali za uzalendo, Ujerumani inajiona ikilazimika kujifunza haraka kujilinda, pia kijeshi.
Lakini hata wapinzani wa kisiasa wa Merkel, kama vile Makamu wa Kansela wa sasa Robert Habeck wa chama cha Kijani, bado wana mtazamo chanya kwa mwanamke aliyeongoza nchi kuvuka mzozo wa sarafu ya euro wa kifedha, pamoja na janga la UVIKO-19. Mnamo Juni, Habeck aliandika kuhusu Merkel katika toleo la Kijerumani la jarida la Rolling Stone kwamba anaweza kumwazia akiwa amekaa nyumbani akimenya viazi au kutazama drama za uhalifu za televisheni. Hii bila shaka ilikusudiwa kuwa pongezi, inayoonyesha namna Merkel anavyichukizwa na aina yoyote ya uovu.