KLABU ya Fountain Gate iko katika hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wa aliyekuwa winga wa Mtibwa Sugar, Kassim Haruna ‘Tiote’.
Nyota huyo wa zamani wa Polisi Tanzania na Namungo kwa sasa ni mchezaji huru baada ya mkataba wake na Mtibwa Sugar kumalizika huku ikielezwa dili la kujiunga na Fountain Gate litakamilisha muda wowote ili akaichezea msimu ujao.
Timu hiyo imekuwa ikipambana kusuka kikosi chake kwa msimu ujao baada ya kumaliza katika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita ikiwa na pointi 33. Msimu uliopita timu hiyo iliyoanza vizuri katika ligi, mwishoni ilianza kupepesuka, lakini ikamudu kubaki Ligi Kuu.
UONGOZI wa JKT Tanzania umeanza mazungumzo ya kumuongezea mkataba mpya nyota wa kikosi hicho, Martin Kigi ili kuendelea kubaki. Hata hivyo, inaelezwa huenda mchezaji huyo akaondoka huku ikielezwa kambi ya nyota huyo haijaridhika na kiwango cha fedha kilichowekwa mezani.
SINGIDA Black Stars huenda ikaachana na mpango wa kumsajili aliyekuwa mshambuliaji wa KenGold, Edgar William msimu ujao. Awali ilielezwa nyota huyo aliyemaliza kinara na mabao 21 Championship msimu uliopita, angejiunga na timu hiyo, japo mmoja wa vigogo inaelezwa alibadili uamuzi na kumuacha akiwa hajui hatima yake.
DODOMA Jiji inakaribia kukamilisha uhamisho wa aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Coastal Union, Ibrahim Ajibu. Nyota huyo wa aliyezichezea Simba, Yanga na Azam FC, kwa sasa ni mchezaji huru na tayari inaelezwa mabosi wa Dodoma Jiji wamekutana na uongozi wa mchezaji huyo ili kuanza mazungumzo ya kukamilisha dili hilo kabla ya wiki hii.