Ligi ya mabingwa Afrika, Yanga kiulaini tu

WAKATI klabu sita zitakazopeperusha bendera ya Tanzania katikamashindano ya klabu Afrika msimu ujao, zimekwepa mtego wa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) baada ya kupata leseni ya ushiriki, upepo mzuri unaonekana kuwa upande wa Yanga inayonolewa na Miguel Gamondi kabla hata mashindano hayajaanza.

Gamondi na jeshi lake wamelainishiwa mapema kulingana na ratiba ya mechi za raundi ya kwanza na zile za pili kama itapenya kufika hatua hiyo na hata itakapokuwa kwenye upangaji wa makundi itakuwa na ulaini kulinganisha na ilivyokuwa msimu uliopita ilipofikia hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Tuanze na ishu ya Leseni za klabu. Taarifa iliyotolewa na Caf imeziwashia taa za kijani, Yanga, Azam na JKU zitakazoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Simba, Coastal Union na Uhamiaji ambazo zitacheza Kombe la Shirikisho baada ya kutimiza vigezo vya kupata leseni ya ushiriki kwenye mashindano hayo msimu ujao.

Vigezo vitatu vikubwa ambavyo timu hizo sita zimetimiza hadi kuhakikishiwa rasmi kuwa zitashiriki mashindano ya klabu Afrika msimu ujao kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Caf ni kuwa na viwanja kwa maana ya uwanja wa mechi na mazoezi, rasilimali watu katika Utawala na kuwa na idara za sheria na fedha.

Idadi ya timu 109 zimefanikiwa kuthibitishwa kushiriki mashindano hayo ambapo timu 58 ni za Ligi ya Mabingwa Afrika na nyingine 51 ni kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.

“Tarehe ya mwisho ya kukusanya taarifa za leseni kwa klabu ilikuwa ni Juni 30,2024,” ilifafanua taarifa hiyo ya Caf.

Katika kundi hilo la timu sita za Tanzania, upepo unaonekana kuiendea vizuri Yanga baada ya kupata taarifa kuwa wapinzani wao Vital’O ya Burundi haitotumia Uwanja wao wa nyumbani wa Intwali kwa mechi za nyumbani kutokana na uwanja huo kutokidhi vigezo.

Timu za Burundi zimekuwa zikitumia viwanja vya Benjamin Mkapa na Azam Complex vilivyopo Dar es Salaam, Tanzania kwa mechi zao za nyumbani jambo linaloweza kuwa la neema kwa Yanga ikiwa Vital’O wataamua kucheza mechi yao ya nyumbani wakiwa Tanzania.

Lakini Yanga ikipenya na kuingia hatua inayofuata, inaweza tena kupata neema ya kutocheza katika nchi husika ambayo mpinzani wake anatokea ikiwa wawakilishi wa Ethiopia, CBE watafuzu mbele ya SC Villa ya Uganda.

Ethiopia haina uwanja ambao utatumika kwa mechi za hatua za mwanzo za mashindano ya klabu Afrika kwa vile Caf haikupitisha viwanja vyake baada ya kukosa sifa ya kutumika kwa mechi za mashindano hayo.

Hilo linailazimu CBE na timu nyingine ya Ethiopia inayoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika kucheza mechi zao za nyumbani katika viwanja vya nchi nyingine.

Bahati nyingine kwa Yanga ni kukosekana kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa baadhi ya timu ambazo zimeizidi pointi katika viwango vya ubora wa Caf, jambo ambalo litaifanya Yanga ipangwe katika chungu cha pili kwenye upangaji wa droo ya hatua ya makundi ikiwa itafanikiwa kuingia hatua hiyo.

Hiyo inamaanisha kuwa Yanga itajiweka kwenye mazingira ya kukwepa wapinzani wengi wagumu kwenye kundi ambalo itapangwa.

Related Posts