AKILI ZA KIJIWENI: Alichokifanya Benchikha sio cha ajabu

WACHEZAJI wawili walioondoka Simba katika dirisha hili la usajili, wamekula maisha huko Algeria baada ya kujiunga na JS Kabylie inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo.

Tunawazungumzia viungo Sadio Kanoute na Babacar Sarr ambao wamemwaga wino wa kuitumikia JS Kabylie msimu ujao, wakiwa wachezaji huru kutokana na sababu tofauti.

Kanoute ameondoka akiwa huru kwani mkataba wake ulikuwa umemalizika na Simba hawakutaka kumuongeza, wakati Sarr yeye mkataba ulivunjwa na Simba kutokana na kutoridhishwa na kiwango chake.

Hapana shaka usajili wa Sarr na Kanoute katika timu ya JS Kabylie umechangiwa zaidi na uwepo wa kocha Abdelhak Benchikha  ambaye ndiye kocha mkuu wa miamba hiyo ya Algeria.

Benchikha aliwafundisha wawili hao wakati alipokuwa akiinoa Simba kabla ya kuachana nayo na kurudi kwao Algeria hivyo ameungana nao tena jambo ambalo linafanya baadhi ya watu nchini kuona kama kuna fungu ambalo kocha huyo kapata kupitia kwa wachezaji hao.

Hata hivyo, kupitia usajili wa Sarr na Kanoute ambao umefanywa na JS Kabylie tunatakiwa kufahamu kwamba makocha wengi wazuri duniani huwa wanapenda kufanya kazi na watu fulani ambao wanafahamiana vyema na wataimba lugha moja iwe wachezaji au maofisa wa benchi la ufundi.

Hiyo inasaidia katika kufanya urahisi kwenye mawasiliano kati ya kocha na kikosi chake kupitia kwa wale ambao amezoeana nao lakini pia anakuwa anafahamu vyema udhaifu na ubora wao hivyo inampa wepesi katika usimamizi wa timu.

Kusajiliwa kwa Kanoute na Sarr pia kunadhihirisha kwamba watatu hao wameishi vizuri ndani ya Simba na wachezaji husika walikuwa na nidhamu, heshima na utii kwa benchi la ufundi hadi kupelekea kujenga imani kubwa ya Benchikha kwao.

Na tusione jambo la ajabu ambalo Benchikha amelifanya na badala yake tulitumie kubadilisha mitazamo yetu kwa kuhisi makocha wanapata cha juu wakisajili wachezaji wao wa zamani.

Related Posts