Rais wa Marekani, Joe Biden jana Jumatano Julai 17, 2024 alipimwa na kugundulika na Uviko-19Â hivyo kulazimika kukatiza mkutano wa kampeni uliokuwa na lengo la kutafutwa uungwaji mkono kwa wapiga kura wa Latino.
Kwa mujibu wa tovuti ya BBC, Biden mwenye umri wa miaka 81 alibainika kuwa na dalili za ugonjwa huo na tayari ameanza matibabu kwa mujibu wa daktari wake.
Hata hivyo, Biden kabla ya kuanza matibabu hayo ambapo pia itamlazimu kujitenga, aliwaambia waandishi wa habari kuwa anajisikia vizuri, japokuwa baadaye alipelekwa katika makazi yake yaliyopo Delaware.
Biden aliwaambia waandishi wa habari Jumatano huko Las Vegas kwamba anajisikia vizuri, huku akionyesha dole gumba kabla ya kupanda Air Force One kuelekea kwenye makazi yake Delaware.
Rais Biden atajitenga Delaware kulingana na mwongozo wa vituo vya Marekani vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa.
Baadhi ya wafuasi wa Chama cha Democratic bado hawana imani na Rais Biden kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi wa mwaka huu ambao una mchuano mkali dhidi ya mgombea wa Republican, Donald Trump.
Mbali na wanachama wenzake kutokuwa na imani naye, lakini pia tukio la jaribio la mauaji ya Rais wa zamani ambaye pia ni mgombea wa Republican, Donald Trump liliongeza joto kwa Wamarekani kumtaka asigombee tena katika muhula ujao.
Saa chache kabla ya Ikulu kutangaza kuwa Biden amegundulika kuwa na Uviko-19, Mwakilishi wa Jimbo la California, Adam Schiff, mgombea wa seneti na mwenyekiti wa zamani wa ujasusi, alikuwa miongoni mwa wanasiasa waliomtaka aachie ngazi hadharani.
Licha ya shinikizo hilo kuwa asigombee, lakini bado Biden ameonyesha msimamo wake ni kugombea nafasi hiyo.