Songwe. Makaburi zaidi ya 30 katika Mtaa wa Majengo, Kata ya Hasanga wilayani Mbozi Mkoa wa Songwe, yamevunjwa kisha kung’olewa misalaba na urembo wa kwenye malumalu.
Mwananchi limefika katika makaburi hayo wakati wananchi wakifanya usafi kwenye makaburi hayo na kushuhudia uharibifu mkubwa katika makaburi hayo yaliyopo eneo la kwa Mzungu.
Akizungumzia hilo leo Alhamisi Julai 18, 2024, mkazi wa Kata ya Hasanga, Merry Kampulo, amesema matukio ya kuvunja makaburi na kuiba vitu vya thamani umeanza hivi karibuni na unazidi kushika kasi katika maeneo hayo.
“Hali hii inatushtua sana hasa sisi wakazi wa kata hizi mbili tunaotumia maeneo haya kuwahifadhi ndugu zetu,” amesema Kampulo.
Anasema kati ya makaburi yaliyobomolewa lipo la mumewe na anasema awali lilivunjwa upande, na leo amekuta limebanduliwa malumalu zote na urembo aliokuwa ameuweka juu ya kaburi hilo.
“Nimesikitika sana, hawa watu wamenirudishia upya majonzi ya kupotelewa na mume wangu …hatujui lengo lao ni nini,” amesema Merry.
Naye Joel Halinga amesema awali walikuwa wakiiba misalaba ya chuma, lakini safari hii wamekuja na wizi mpya wa kubandua malumalu na mikanda inayotumika kuunganishia malumalu zisiweze kubanduka baada ya kujengwa.
Mkazi wa Kijiji cha Hasanga, Audela Kashasha ambaye pia kaburi la mtoto wake limebanduliwa malumalu alizozijengea tangu mwak 2018, anasema kama wamefikia hatua ya kubandua malumalu, huenda kuna siku wakayafukua makaburi hayo.
“Kama wanaharibu makaburi hivi, hofu yetu ni kwamba, huenda baadae wataanza kufukua mpaka miili ya wapendwa wetu, tunaiomba Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama watusaidie kuwatafuta na kuwachukulia hatua kali ili kukomesha kabisa vitendo hivi,” amesema Kashasha.
Mwananchi ilimtafuta Mwenyekiti wa Mtaa wa Ichenjezya, Enock Kalonge amesema baada ya kubaini uharibifu huo tayari wameshatoa taarifa kwa viongozi wa kata.
“Lakini kwa hatua za awali tumeamua kufanya usafi wa kufyeka na kukwetua eneo la makaburi na tumewashirikisha wazee wa mila na tumewajulisha viongozi ngazi ya wilaya kuhusiana na hili,” amesema Kalonge.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, George Msyani amekiri kutokea kwa tukio hilo na kukemea huku akiwataka wananchi kuendelea kuimarisha ulinzi na kutokomeza vitendo hivyo ambavyo vinaharibu taswira katika jamii.
“Pia tuwasake watu hawa ili kuwabaini na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao,” amesema mwenyekiti huyo.