Mbunge ‘ashtaki’ kwa Rais Samia wananchi kukosa vitambulisho Nida

Dar es Salaam. Mbunge wa Momba (CCM), Condester Sichalwe amemweleza Rais Samia Suluhu Hassan kilio cha wananchi kuhusu changamoto ya upatikanaji wa Vitambulisho vya Taifa katika Mkoa wa Songwe.

Sichalwe amebainisha hayo leo Alhamisi Julai 18, 2024 Tunduma mkoani Songwe wakati wa ziara ya Rais Samia katika mkoa huo ambapo alisimama kuzungumza na wananchi na viongozi wa mkoa kupata nafasi ya kuzungumza.

Mbunge huyo ameeleza wananchi wa Songwe wamekuwa wakilalamika kutopata vitambulisho vya Taifa vinavyotolewa na mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), hivyo wanakwama kupata baadhi ya huduma muhimu.

Ameshauri vitambulisho hivyo vinaweza kutolewa sambamba na shughuli ya uandikishaji wapigakura kwenye eneo hilo ili kurahisisha maisha ya wananchi wa Tunduma na mkoa mzima wa Songwe.

“Ombi langu kwako mama, wakati tutakuwa tunazindua daftari la wapigakura, tunaomba waweze kuandikisha na vitambulisho vya Nida. Kuna watu wa Tasaf wanashindwa kupata huduma kwa sababu ya vitambulisho vya Nida,” amesema Sichalwe.

Akijibu changamoto hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo hasa kwa wananchi waishio pembezoni na kueleza kwamba tatizo hilo linakwenda kuisha kutokana na mipango iliyopo.

Amesema wakati Rais Samia anaingia madarakani, alikuta deni la mkandarasi la Sh7.5 bilioni lakini amelipa zote. Amesema Serikali imetoa Sh2.5 bilioni kwa ajili ya kununua kadi zinazowatosha Watanzania wote nchini na tayari zingine zimepelekwa Songwe.

“Maeneo ya mipakani yana mwingiliano mkubwa na watu wa nchi jirani. Hivyo unafanyika uhakiki wa raia ili tujue nani anapewa kitambulisho, hili ni muhimu sana kwa usalama wa Taifa,” amesema Masauni.

Hata hivyo, amesema Serikali imezindua mkakati maalumu wa utoaji vitambulisho kwa wananchi waishio mipakani na kwamba mambo yatakuwa mazuri yakifanyika mabadiliko ya mfumo wa utendaji wa Nida.

“Tumeanza kuzitatua changamoto hizo hatua kwa hatua. Mtakumbuka Rais alitupa ushauri wa kuwa na namba moja ya utambulisho wa Mtanzania. Mambo haya ni muhimu kuyafanyia utafiti kuangalia muundo na utendaji kazi wa Nida kwa ujumla wake.

“Mambo haya yanahitaji mabadiliko ya sheria. Kamati iliyokuwa kazini, imemaliza kazi yake. Tunataka chombo hiki kifanye kazi yake kwa ufanisi ili kupunguza malalamiko ya wananchi,” amesema Waziri Masauni.

Awali, Mbunge wa Tunduma (CCM), David Silinde ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo, amemshukuru Rais Samia kwa miradi mingi aliyoipeleka katika mji huo kwani amewaponya na maombi yote aliyoyapeleka kwake ameyatekeleza kwa asilimia 100.

“Kwenye elimu, tulikuomba ukatuletea shule za kumwaga, sasa hivi umetuletea shule saba, tumezijenga na nyingine ni za ghorofa. Tumetumia pesa zetu za ndani kuongeza kujenga madarasa ya ghorofa.

“Kwenye afya, umetupatia vituo vitano kwenye mji wa Tunduma, kila kona ukienda kuna kituo cha afya. Upande wa barabara, wakati unaingia madarakani mji wa Tunduma ulikuwa na kilomita 1.2 za barabara za lami lakini sasa tuna barabara ya kilomita 10.2,” amesema.

Ameongeza kuwa kwenye umeme, hatukuwa na umeme lakini sasa hatukudai kitu, kwenye mitaa yote umeweka umeme.

Related Posts