16 wahofiwa kuambukizwa kipindupindu Morogoro

Morogoro. Wakazi wa Manispaa ya Morogoro wanahofia kukumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu huku wagonjwa 16 wanaodhaniwa kuwa na ugonjwa huo wakilazwa katika Kituo cha Afya cha Sabasaba.

Mganga Mkuu wa kituo hicho kilichopo Manispaa ya Morogoro ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake, amesema Julai 16 na 17, 2024, hospitali hiyo imepokea wagonjwa wa kuharisha na kutapika zaidi ya 15.

“Juzi na jana tulipokea wagonjwa wengi wa kutapika na walianza kuja watano lakini hadi jioni tulikua na wagonjwa 15 ambao walikuwa wakiharisha na kutapika, baada ya kuchukua sampuli na kuzipeleka maabara tuligundua wana viashiria vya maambukizi ya kipindupindu.

“Kwa hiyo, hadi leo Julai 18, 2024, tuna wagonjwa 16 ambao tunaendelea kuwahudumia kwenye hospitali yetu,” amesema.

Amesema tangu Januari 2024 wakati wa mvua za masika na maeneo mengi kukumbwa na mafuriko, kumekuwa na wagonjwa wa kuharisha na kutapika na kwa hali iliyopo, lazima jitihada za makusudi zifanyike ili kukabiliana na ugonjwa huo.

Meya wa Manispaa ya Morogoro, Pascal Kihanga amesema manispaa hiyo kupitia kwa Ofisa Afya wa Manispaa, wameagiza timu ya wataalamu kuchunguza kuhusu ugonjwa huo uliowakumba baadhi ya wananchi kwani hakuna kweli wowote kuwa ni kipindupindu.

“Jana, ofisa afya ametoa taarifa ya kuwa ule ugonjwa sio kipindupindu na ni vizuri kuheshimu taaluma yake maana yeye ndio mtaalamu wa hayo mambo na  kwa sasa bado wanafanya utafiti ili kugundua ni ugonjwa gani na chanzo chake ni nini,”  amesema.

Amesema kipindupindu kinaweza kutokea katika majira haya ya kiangazi, hivyo kinachofanyika kwa sasa kupitia wataalamu wa manispaa ni kungojea uchunguzi ili kujua ugonjwa huo ni wa aina gani na dalili zake ni zipi kwa kuwa maana umezuka ghafla,” amesema Kihanga.

Mkazi wa Kihonda, Deus Zephania amesema anaishi na ndugu yake ambaye naye siku mbili zilizopita alimpeleka hospitali akikabiliwa na changamoto ya kutapika na kuharisha, hata hivyo hakuwa anafahamu huo ni ugonjwa gani.

“Nimempeleka mdogo wangu Kituo cha Afya cha Sabasaba kupatiwa matibabu baada ya kuanza ghafla kuharisha na kutapika kwa pamoja. Ilitushtua lakini alipokwenda hospitali, alipewa matibabu na kwa sasa anaendelea vizuri, kwa maana hiyo tunawaomba Serikali watusaidie kuweka mazingira safi na salama ili tuepukane na haya magonjwa,” amesema Zephania.

Related Posts