Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam imemuhukumu kijana Samwel Gombo kutumikia kifungo cha miaka mitano gerezani na kulipa fidia ya zaidi ya Sh. Milioni 100 baada ya kupatikana na hatia ya kughushi cheti cha kifo cha baba yake wa kambo
Aidha mahakama imemuachia huru Musa Yohana aliyekuwa anashtakiwa pamoja na Gombo baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yake.
Katika kesi hiyo Gombo alikuwa anakabaliwa na shtaka la wizi, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu wakati Yohana alikuwa anakabiliwa na shtaka la kughushi peke yake.
Hukumu hiyo imesomwa leo Julai 18, 2024 na Hakimu Mkazi Mkuu Ushindi Swalo baada ya kuridhika na ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo ikiwemo cheti cha kifo, muhtasari wa kikao cha mirathi cha familia hati ya uwakilishi ya ya akaunti ya marehemu ya benki.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Swalo amesema mshtakiwa ametiwa hatiani baada ya kosa lake la wizi kuthibitika amesema, ni kosa kisheria kutumia fedha za marehemu kwa madai kwamba kulikuwa na wosia mshtakiwa hakuwa na mamlaka yoyote ya kutumia fedha za marehemu na wala hakuwa na dai la haki badala yake amewadhulumu wote waliokuwa na haki ya kupata fedha hizo hivyo.
Mapema katika ushahidi wake, mshtakiwa alidai aliichukua fedha hiyo sababu marehemu baba yake aliacha wosia kwamba hizo fedha zote alishammilikisha ni za kwake
Hata hivyo mahakama imemtia hatiani kwani mshtakiwa alishindwa kuleta huo wosia ambao alidai wakili Dickson Matata ndio alikuwa anautunza wosia huo lakini alishindwa kumleta mahakamani wala wosia wenyewe kuthibitisha kuwa kweli yeye alimilikishwa fedha hizo kabla hajafa.
Hata hivyo kabla ya kusoma hukumu hiyo Hakimu Swalo aliuliza upande wa mashtaka kama walikuwa na lolote la kusema ndipo wakili wa serikali Asiath Mzamilu akadai hana kumbu kumbu ya makosa ya nyuma ya mshtakiwa ila ameiomba mahakama kumpa adhabu kwa mujibu wa sheria
Katika utetezi wake, mshtakiwa aliiomba mahakama impunguzie adhabu kwa kuwa hilo ni kosa lake la kwanza na pia familia inamtegemea.
Awali ilidaiwa kuwa, Stanford Gombo aliyekuwa baba wa mshitakiwa Samwel, alifariki Novemba 11 mwaka 2017 na kuzikwa Novemba 13 mwaka huo ambapo aliacha mali mbalimbali ikiwemo Sh. 102,900,784 katika benki ya NMB.
Ilidaiwa kwamba mwaka 2019 familia ya Stanford ilikaa kikao cha familia na kumteuwa Yared Gombo kuwa msimamizi wa mirathi.
Kwamba mshitakiwa Samwel alibaki na kadi ya Stanford na hakutaka kusema kama anayo licha ya wanafamilia kuitafuta.
Ilidaiwa kwamba, kati ya Novemba 13 mwaka 2017 hadi Juni 30 mwaka 2018, Dar es Salaam, Samwel alichukua fedha hizo benki katika akaunti ya baba yake.
Iliendelea kudaiwa mshitakiwa huyo aligushi muhtasari wa kikao cha familia, cheti cha kifo cha baba yake akionesha kimetolewa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) na nguvu ya kisheria na kuiwasilisha mahakama ya mwanzo Chakwale ,Wilaya ya Gailo , Morogoro.
Kwamba Mei 6 mwaka 2022, washitakiwa hao walikamatwa na kufikishwa mahakamani.