Kopunovic atoa masharti nyota sita Pamba

LICHA ya uongozi wa Pamba Jiji kukamilisha usajili wa wachezaji 24 hadi sasa, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Goran Kopunovic amesema anahitaji wachezaji sita wenye ubora wa kucheza Ligi Kuu na kuisaidia timu hiyo kutoa ushindani kwani michuano hiyo ni migumu.

Pamba Jiji iliwaongezea mikataba wachezaji saba wa msimu uliopita na imeshatangaza wachezaji wapya 17 na mwishoni mwa wiki iliyopita ilifanya mazoezi ya mwisho katika Uwanja wa Nyamagana, jijini hapa na Jumatatu ikasafiri kwenda Morogoro kuanza kambi ya wiki mbili ikiwa na wachezaji 20.

Kopunovic alisema tangu alipotua klabuni hapo mwanzoni mwa Julai amewaona wachezaji wengi waliokuja kwenye majaribio na kufanya usajili wa wachezaji 20, hivyo haitaji wachezaji wengine wa majaribio.

Alisema raundi ya kwanza Ligi Kuu anaanza na kikosi cha wachezaji 26 kisha kama kutahitajika mabadiliko watafanya dirisha dogo, huku nafasi sita zilizobaki akiwataka nyota wa daraja la juu na watakaoshindana Ligi Kuu na kuingia kikosini moja kwa moja.

“Bado tunatafuta wachezaji wenye ubora baadhi ya nafasi, timu ya wachezaji 26 inatosha kwa kuanzia kisha tutaona raundi ya kwanza nini kitatokea, vitu gani nataka, nidhamu na kuwajua wachezaji alafu tutaangalia labda Januari (dirisha dogo) kuleta mabadiliko.”

“Lakini kwa sasa tunahitaji kuongeza wachezaji watano ama sita wa ubora wa juu watakaoingia kikosini moja kwa moja, siwezi kuahidi matokeo mazuri, ninachoahidi kwa mashabiki wa Pamba Jiji ni naandaa timu ya kucheza soka safi na la kisasa.”

“Kila mtu anapaswa kuelewa Ligi ya Championship na Ligi Kuu ni vitu viwili tofauti, kwa timu mpya inayoingia Ligi Kuu ni mtihani mkubwa tunapaswa kuwa makini sana. Lazima tuwe na timu ya kushindana na tucheze soka la kisasa ili tuibakishe timu Ligi Kuu,” alisema Kopunovic.

Related Posts