Ikihitimisha mkutano mkuu wa kihistoria wa chama hicho uliokumbwa na jaribio la kutaka kumuua la mwishoni mwa wiki iliyopita.
Rais huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 78 anaweza kutarajia makaribisho ya kishujaa katika siku ya mwisho ya Kongamano la Kitaifa la Republican mjini Milwaukee, anapohutubia taifa linaloendelea kukumbwa na mshtuko kutokana na jaribio la mauaji dhidi yake, katika mkutano wa hadhara jimboni Pennsylvania.
Soma pia:Trump apokelewa kwa shangwe na Waprepublican
Shambulio hilo la Jumamosi, ambalo lilimuua mtu mmoja aliyesimama karibu na kumjeruhi sikioni Trump, limeugubika mkutano huo, huku Warepublican wakijitokeza kumsifu rais huyo wa zamani kwa ushujaa wake.
Huku baadhi ya Warepublican wakitaka kulaumu matamshi ya Wademokrat dhidi ya Trump kuchochea shambulio hilo, bilionea huyo alisema amechana hotuba yake ya awali iliyokuwa na maneno makali zaidi na kuandaa nyingine ambayo anatumai itasaidia kuiunganisha nchi.
Akijivunia mafanikio ya kuaminiwa pakubwa na wakereketwa wa chama hicho, Trump ameshuhudia uongozi wake katika uchunguzi wa maoni ya raia ukipanuka tangu utendaji mbaya wa rais Joe Biden kwenye mdahalo wa televisheni mwezi uliopita, ulipoibua mzozo mkubwa ndani ya chama cha Democratic.
Mbinu ya kupenya katika ngome za upinzani
Kampeni yake imekuwa ikizungumza hata uwezekano wake kupenya katika ngome za chama cha Democratic kama vile Minnesota na Virginia, hali inaweza kuilaazimu timu ya Biden kuhamisha fedha na nguvukazi kutoka kwenye utetezi wa ukuta wake wa bluu katika majimbo ya Michigan, Pennsylvania na Wisconsin.
Hotuba ya leo ya Trump itafuatiliwa kupitia televisheni na mamilioni, akifunga mkutano huo mkuu kwa kukaribisha kile ambcho timu yake ya kampeni imekitaja kuwa zama mpya ya dhahabu kwa Marekani.
Itahitimisha siku nne za hotuba kutoka kwa maafisa wa kuchaguliwa, viongozi wa kisekta na Wamarekani wa kawaida waliochanganyika na Wrepublican elfu 50 waliosafiri kutoka maeneo yote ya nchi.
Mkutano huo ulifunguliwa Jumatatu kwa uwanja uliojaa wa wajumbe, ambao ni mchanganyiko wa wanasiasa na wanaharakati wa mashinani, wakipiga kura kumthibitisha Trump kama mteule baada ya kushinda karibu kila kura ya mchuji katika majimbo.
Soma pia: Trump amchagua Seneta JD Vance kama mgombea mwenza
Trump aliunda hali ya mkutano huo mkuu alipoingia kwenye Jukwaa la Fiserv siku ya ufunguzi, akionekana mwenye hisia na sikio lililofungwa bendeji, baada ya kumtangaza Seneta wa mrengo wa kulia J.D. Vance kama mgombea mwenza wake.
Vance mwenye umri wa miaka 39 na mwandishi wa kitabu kilichoweka rekodi ya mauzo cha Hillbilly Elegy, kuhusu kukulia kwenye familia maskini ya wafanyakazi wa vijijini, aliwa mkosoaji mkubwa ambaye amegeuka mmoja wa wafuasi sugu wa Trump.
“Rais Trump anawakilisha tumaini bora la mwisho la Marekani kurejesha kile ambacho ikikipoteza kinaweza kisipatikane tena – nchi ambayo kijana wa tabaka la wafanyakazi aliyezaliwa mbali na kumbi za mamlaka anaweza kusimama katika hatua hii kama makamu wa rais ajaye wa Marekani.”
Biden azidi kuelemewa
Wakati Trump anazidi kujiamini kurejea kwa njia ya kushangaza katika Ikulu ya White House, licha ya matatizo mengi ya kisheria na mashitaka mawili yaliyougubika muhula wake wa kwanza, Rais Joe Biden anakabiliwa na anguko kubwa la umaarufu wake na wasiwasi wa chama chake kuhusu afya yake.
Akiwa na umri wa miaka 81, Biden amekuwa akikabiliwa na miito inayoongezeka kutoka chama chake kujiengua kwenye uchaguzi kutokana na wasiwasi wa umri wake, na wiki yake ilizidi kuwa mbaya zaidi Jumatano alipogunduliwa na maambukizo ya virusi vya UVIKO-19.
Soma pia: Rais Biden alazimika kusitisha kampeni zake
Trump mwenyewe alidhoofika baada ya kushindwa kwake katika uchaguzi wa 2020 na ghasia zilizofanywa na wafuasi wake dhidi ya majengo ya bunge, lakini ametumia muda mrefu wa miaka minne iliyopita kuunda upya siasa za Republican.
Akiweka wafuasi waaminifu, akiwemo mke wa mtoto wake Lara Trump katika uongozi wa Kamati ya Taifa ya chama cha Republican, tajiri huyo kimsingi amezima upinzani wowote ndani ya chama.
/AFP