Mikakati ya GBT katika mapambano dhidi ya mashine haramu za sloti ‘Dubwi’

Michezo ya kubahatisha inajumuisha michezo ya aina mbalimbali ikiwemo Bahati Nasibu ya Taifa, kasino, michezo ya kubashiri matokeo (sports betting), michezo inayotumia jumbe fupi (SMS Lottery) na michezo ya kutumia mashine za sloti ama kwa jina maarufu huko mtaani “Dubwi”.

Dhana kubwa ya michezo yote ya kubahatisha ni burudani na kushinda ni kwa bahati tu.  Endapo itatumika kinyume cha hapo inaweza kuwa na madhara kama ya utegemezi na uraibu.

Sekta ya michezo ya kubahatisha imekuwa ikikua kwa kasi sana katika miaka ya hivi karibuni. Ili kuiwezesha sekta hiyo kuwa na tija na kuzuia matokeo hasi kwa jamii, mnamo mwaka 2003 Serikali iliunda chombo maalum cha kusimamia na kudhibiti uendeshaji wa sekta hiyo ambacho ni Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) kwa lengo la kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika kiuchumi pasi na kuleta madhara katika jamii.

Washiriki kutoka tasnia ya michezo ya kubahatisha wakiwa katika picha ya pamoja mbele ya banda la GBT katika Maonyesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba, 2024) waliyoshiriki ili kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na uendeshaji, usimamazi na uchezaji wa busara na salama wa michezo ya kubahatisha.

Chini ya usimamizi wa GBT, Serikali na jamii imepata mafanikio lukuki ikiwemo kuongezeka kwa mapato mwaka hadi mwaka na kuchochea maendeleo katika utoaji wa huduma na kukuza michezo.

Mathalani katika mwaka wa fedha 2022/23 mapato yatokanayo na kodi katika sekta ya michezo ya kubahatisha yaliongezeka na kufikia Sh170.43 bilioni kutoka Sh148 bilioni zilizokusanywa katika mwaka wa fedha 2021/22 ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.2.

Mbali na mapato, sekta ya michezo ya kubahatisha pia imekuwa ikichangia kwa kiasi kikubwa katika kutoa ajira kwa Watanzania na kuleta fedha za kigeni. Pamoja na mafanikio hayo, sekta hii inapitia changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya watu wasio waaminifu kuendesha biashara ya michezo ya kubahatisha bila kufuata sheria na taratibu.

Hivi karibuni kumeibuka wimbi la baadhi watu kuweka na kutumia mashine za sloti maarufu “dubwi” kiholela kwenye maeneo yasiyoruhusiwa na bila kusajiliwa na GBT. Hali hii inasababisha upotevu wa mapato ya Serikali, kuchochea ushiriki wa watoto na kuleta kero kwa jamii pamoja na kuharibu taswira ya sekta ya michezo ya kubahatisha kwa ujumla hapa nchini.

Kwa kuzingatia hali hiyo, Julai 2023 GBT ilianzisha kampeni maalum dhidi ya waendeshaji wote haramu wa biashara ya mashine za sloti inayoitwa “Fichua, Tukomeshe Mashine Haramu”.

Akiongea kutoka katika banda la GBT wakati wa Maonyesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (SabaSaba), Afisa Mwandamizi wa Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa GBT, Zena Athumani anasema “Fichua, Tukomeshe Mashine Haramu” ni kampeni yenye lengo la kukomesha uendeshaji usiofuata sheria na taratibu wa mashine za sloti “dubwi” kote nchini.

“Kampeni hii ni endelevu na ilianza tangu Julai, 2023. Kampeni imejikita katika maeneo makuu manne ambayo ni; kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu michezo ya mashine za sloti ili waweze kutambua sehemu zinazoruhusiwa na zisizoruhusiwa kuwekwa mashine hizo, kuunda ushirikiano na wananchi katika kutoa taarifa za waendeshaji haramu wa mashine hizo, kuzuia ushiriki wa watoto na vijana wenye umri chini ya miaka 18 katika michezo hiyo, kuwaelewesha wananchi taratibu za uendeshaji wa michezo hiyo ili wafahamu kwamba iko chini ya sheria na inadhibitiwa na GBT,” anasema Zena.

Katika mkakati wa kufanikisha kampeni hiyo dhidi ya kuzagaa kwa mashine haramu za Dubwi nchini, GBT imekuwa ikitumia vyombo mbalimbali vya habari kuongea na wananchi moja kwa moja katika maonyesho ya Sabasaba na pia kuwashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama.

Aidha Zena alisema kuwa GBT imepanga kufanya semina na wenyeviti wa Serikali za mitaa wa Mkoa wa Dar es Salaam hivi karibuni ili kuwaelimisha na kuwawezesha kutoa ushirikiano katika kufanikisha kampeni hii.

“Kukabiliana na mashine haramu za sloti “Dubwi” mitaani ni jambo linalohitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali, hivyo ni muhimu kupata ushirikiano kutoka kwa Serikali, wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama,” anasema Zena.

Mbali na hatua hiyo, GBT imejidhatiti kuhakikisha kuwa inawekeza katika teknolojia ili kubaini mashine haramu ili ibaki katika dhamira ya kuwepo kwake na kusukuma gurudumu la maendeleo ya nchi.

Afisa Mkuu wa Ukaguzi kutoka Idara ya Ukaguzi na Udhibiti ya GBT, Emmanuel Ndaki anasema, mashine za Dubwi kisheria zinaruhusiwa kuwekwa katika maeneo mawili tu; kwenye maeneo yanayouza vileo (baa, grosari na klabu za usiku) pamoja na kwenye maduka maalum ya kuchezea mashine hizo yaani Slot Shops. Tofauti na maeneo hayo, biashara hiyo itakuwa ni haramu na inaendeshwa kinyume cha sheria.

“Ili mtu aweze kuendesha mashine hizi anatakiwa kuwa na leseni mbili ambazo ni; leseni kuu (principal license) ambayo inamruhusu kuendesha michezo ya mashine za sloti hapa nchini Tanzania, na nyingine ni leseni ya eneo husika la kuendeshea biashara ya mashine hizo (site license)” anasema Ndaki.

Anasema lengo la sheria kuainisha maeneo hayo mawili kuwekwa mashine za sloti au kama zinavyojulikana kwa jina la mtaani la Dubwi, ni ili kuzuia watoto au vijana wenye umri chini ya miaka 18 kuweza kuzifikia na kucheza kwenye mashine hizo kwa kuwa kisheria hawaruhusiwi kufika katika maeneo hayo.

Ndaki anasema, wanaoendesha biashara ya mashine za sloti “Dubwi” zisizokuwa na usajili (haramu) wanaweza kubainika kwani hawana leseni hai ya biashara na vibali vya kufanyia biashara mahali ilipo mashine kwa wakati huo na stika maalum za GBT.

Akielezea mafanikio ya kampeni hiyo Ndaki anasema kumekuwa na mafanikio makubwa katika utekelezaji wake tangu ilipoanzishwa mwaka mmoja uliopita.

“Katika mwaka wa fedha 2022/23 tumefanikiwa kukamata mashine haramu 363 pamoja na kukusanya faini ya Sh88.7 milioni zilizotokana na makosa hayo. Aidha katika mwaka wa fedha 2023/24 tumefanikiwa kukamata mashine 715, watuhumiwa 27 pamoja na kukusanya faini ya Sh236.7 milioni,” anasema Ndaki.

Aliongeza kuwa GBT wanapokamata mashine hizo, wanafuata utaratibu wa kuziteketeza katika maeneo maalumu yaliyoelekezwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) ambapo gharama zote za zoezi hilo zinalipwa na aliyekutwa na mashine hizo.

“Mbali na adhabu ambazo watuhumiwa wanapewa ikiwemo kulipa faini, na kulipa fidia ya kodi katika kipindi chote walichoendesha mashine hizo kinyume cha sheria, lakini pia wanatakiwa kulipia gharama za uteketezaji wa mashine hizo,” anasema Ndaki.

Mratibu Mkuu wa kampeni hiyo, Zena, ametoa wito kwa watu wote wanaoendesha biashara ya mashine hizo kiholela bila kuwa na leseni na pia kuziweka sehemu zisizoruhusiwa kama vile mbele ya maduka ya mangi, saluni, kwa mama lishe, kwenye vibaraza vya nyumba au vichochoroni, kuacha mara moja kufanya hivyo na kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayekutwa anaendesha biashara hiyo kiholela.

Aidha, Zena amewasihi wananchi kutoa taarifa GBT endapo wataona wamiliki wa mashine za sloti “Dubwi” wakiendesha shughuli zao bila ya vibali au kuchezesha katika maeneo yasiyoruhusiwa na kuruhusu watoto kucheza.

Taarifa hiyo itolewe kupitia simu ya bure namba 0800 11 00 51 au kupitia barua pepe: [email protected] au kwenye kituo cha polisi kilichopo karibu au kufika ofisi za GBT Dodoma na Dar es Salaam kwenye jengo la Kambarage ghorofa ya 3 au majengo pacha ghorofa ya 27 mtawalia.

Iwapo jamii itashikamana katika mapambano dhidi ya mashine haramu za sloti ama Dubwi au uvunjifu mwingine wa sheria, kanuni na miongozo iliyopo na wachezaji wakaelewa dhana nzima ya michezo ya kubahatisha kuwa ni burudani wala siyo kazi au chanzo rahisi cha kipato, Taifa litanufaika kupitia michezo hiyo kwa mapato na kuinua maisha ya wananchi.

Related Posts